Butiama, Musoma wanapeta tu na sensa

WAKUU wa wilaya za Butiama na Musoma mkoani Mara wamesema hadi sasa sensa ya watu na makazi inafanyika vizuri na wameomba wananchi ambao hawajafi kiwa wawe wavumilivu.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mwalimu Moses Kaegele alisema hadi jumatano mchana hakuna mtu aliyegoma kuhesabiwa au kukwamisha kazi hiyo.

“Bado tuna siku za kufanya kazi hii na hivyo nawataka wananchi watakapofikiwa na makarani, wawape ushirikiano ili tumalize vizuri,” alisema Kaegele.

Alishauri wananchi waendelee kutunza taarifa zao vizuri ili kurahisisha kazi na watoe taarifa sahihi.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Khalfan Haule alisema shughuli hiyo imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi, tangu wakati wa mafunzo kwa makarani mpaka jana hakukuwa kumetokea kikwazo chochote kwa wananchi wala makarani.

“Ingawa sipo kwenye nafasi nzuri ya kukupatia takwimu za watu na kaya zilizohesabiwa tangu jana mpaka sasa, lakini wananchi wamekuwa na mwitiko mzuri na makarani wanazingatia utaratibu kutimiza majukumu yao vizuri,” alisema Dk Haule katika mahojiano na gazeti hili.

Aliomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa makarani wanapowafikia na kwa wanaoondoka waache taarifa nyumbani, kwa majirani au kwa kiongozi wa mtaa kama hakuna anayebaki nyumbani

Habari Zifananazo

Back to top button