Butiama, Musoma wapongeza ushirikiano wa wananchi

WAKUU wa Wilaya za Butiama na Musoma mkoani Mara, wamesema, mpaka sasa sensa ya Watu na Makazi inafanyika vizuri na wameomba wananchi ambao hawajafikiwa, wawe wavumilivu kwasababu kazi hiyo inaendelea mpaka Agosti 29, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mwalimu Moses Kaegele amesema kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini, kazi hiyo ilianza jana Agisti 23, 2022 na mpaka sasa hakuna mtu aliyegoma kuhesabiwa au kukwamisha kazi hiyo.

“Tunaomba ambao hawajafikiwa waendele kuvumilia kwakuwa bado tuna siku sita za kufanya kazi hii na watakapofikiwa na makarani, wawape ushirikiano ili tumalizevizuri,” amesema DC Kaegele.

Pia ameshauri wananchi waendelee kutunza taarifa zao vizuri, ili kurahisisha watakapofikiwa iwe rahisi kwao kufanya mahojiano kwa haraka na usahihi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Khalfan Haule amesema shughuli hiyo imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi, tangu wakati wa mafunzo kwa makarani mpaka sasa hakujatokea kikwazo kutoka kwa wananchi wala makarani.

Amewaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa makarani wanapowafikia na kwa wanaoondoka nyumbani wameombwa kuacha taarifa kwa wanaobakia nyumbani ambao ni wakubwa na wenye uwezo wa kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa hiyo.

Amesema ikiwa hakuna anayeachwa nyumbani mwenye uwezo huo, taarifa zinaweza kuachwa hata kwa jirani, lakini pia inashauriwa kuweka hata namba za simu, ili karani akihitaji ushirikiano zaidi, aweze kuwasiliana na muhusika.

Habari Zifananazo

Back to top button