DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Mwanasiasa Mkongwe, Joseph Butiku amesema Muungano sio kwaajili ya viongozi na vyama vya siasa bali kwaajili ya wananchi wote ni hivyo kila mtu anapaswa kushiriki.
Butiku amesema lengo la Muungano ni kujenga umoja na kuondoa unyonge hali iliyofanya waweze kujitawala.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la miaka 60 ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanywa na Chuo cha Ustawi wa Jamii ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha muungano Butiku amesema Wananchi walikubali kwa kushawishiwa na kujenga nguvu ili kuondoa unyonge ulikuwa hiari,wamazungumzo.
“Napenda muelewe kuwa muungano sio wa Nyerere wala wa Karume wala sio wa Samia wala CCM ni wa wananchi wa Tanzania wale ni viongozi walioonesha njia na wananchi wakakubali hivyo muungano ni wazanzibar na watanganyika waliokubaliana kutokana na uongozi na watu wanao uhuru wao na wao wanaendelea kuwaongoza ndio maana muungano wetu ni wa nchi mbili ,”amesisitiza.
Amesema kuelewana kati ya Karume na Nyerere ilikuwa kazi kubwa na kuanza mgawanyo wa madaraka polepole na hata sasa Rais Samia anakwenda pole pole .
“Sera ya TANU ilikuwa serikali mbili kwenda serikali moja na baadae wakaona sio busara twende hivi hivi na tuko nchi mmoja tujenge hili katika vizazi vyetu ila serikali ni mbili wote tufanye kazi kwani bila kufanya kazi hakuna umoja na muungano.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni amesema wameandaa kongamano hilo ili kujadili kuhusu muungano ambapo wameona kuna umuhimu kuwajengea uwezo wanafunzi kujua muungano na kuwa sehemu ya kuunga mkono hata kwa kizazi chao.
“Tumekuwa na watu mbalimbali wanaofundisha akiwemo mwanasiasa mkongwe mzee Butiku kila mtu anao wajibu kuhakikisha na kujiona kama sehemu ya muungano kama chuo tunawajibu wa kufundisha vijana kuona kama wao ni sehemu ya muungano na tumeweza kuakisi mtaala utakaojenga uelewa kwa wanafunzi.