KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira inatarajia kukaa na kuchakata maoni na ushauri iliopokea kutoka kwa watalaamu kuhusu nia ya Wizara ya Maji kutumia maji ya Bwawa la Mtera kupunguza tatizo la upungufu wa maji jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, kutokana na wingi wa watu unaotokana na serikali kuhamia katika jiji hilo, Dodoma kuna upungufu wa maji unaofikia lita milioni 65 wakati inazalisha lita milioni 68 na mahitaji ni lita milioni 133 za maji.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kamati hiyo kuona maendeleo ya bwawa hilo la Mtera, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga alisema baada ya kuchakata maoni ya wataalamu hao kamati hiyo itatoa ushauri utakaozingatia mahitaji ya wananchi wa Dodoma.
Alisema kazi kubwa ya Kamati ya Bunge ni kushauri, hivyo ziara hiyo ililenga viongozi hao kuona hali halisi ya maji ya bwawa la Mtera na kujiridhisha.
Alisema katika ziara hiyo, wamesikiliza watalaamu wakiwemo wa Wizara ya Maji na wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanaotumia maji ya bwawa hilo kuzalisha umeme na kisha watachakata maoni yao na kushauri nini kifanye kwa manufaa ya watu wote.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema Dodoma maji yapo lakini si toshelevu sababu mahitaji ni lita milioni 133 hadi 134.
Alieleza kuwa wizara hiyo inaamini katika ushirikishwaji ndio maana wameishirikisha Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira, Wizara za Nishati, Mazingira na Fedha ili kuja kuona wazo hilo.
“Timu ya ushauri ipo kazini kufanya tathmini kwa wazo hili tunalowaza, utekelezaji wake upoje, je, kuna athari gani na tunaweza kudhibiti vipi,” alisema.
Aweso alisema bwawa hilo lina uwezo wa kuzalisha maji lita bilioni 3.7 wakati Dodoma itahitaji lita milioni 130 na inawezekana kuchukua zaidi ya hapo kwa sababu yapo ya kutosha kinachohitajika ni kujaziliza.
“Hatuwezi kuwekeza fedha kwa kukurupuka maana yake tuna wataalamu wanafanya tathimini, mwisho wa siku sisi kama viongozi mawazo yote tutakayoamua yatakuwa na manufaa kwa taifa na wananchi kwa ujumla,” alisema.
Awali, akitoa taarifa fupi ya kituo cha kufua umeme cha Mtera, Meneja wa kituo cha Mtera, Edmund Seif alisema kupitia kituo hicho Tanesco wana mashine mbili zinazoendeshwa kwa nguvu ya maporomoko ya maji zilizofungwa ndani ya mgodi zenye uwezo wa kuzalisha umeme megawati 80 kwa saa.
Alisema kituo hicho kina uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo bilioni 3.7 linapokuwa limejaa na maji hayo hutumika kuzalisha umeme kwenye vituo vya Mtera na Kidatu.
Alieleza kina cha bwawa cha chini cha uzalishaji ni mita 690.00 juu ya usawa wa bahari na linategemea vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni mto Ruaha Mkuu, Ruaha Mdogo na Kisigo.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kina cha maji kinapofikia mita za ujazo 690.00 kituo hicho hulazimika kuzima mitambo yake kwa kuwa maji yanakuwa yako chini sana na ni hatari kwa mashine zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji wa Wizara ya Maji, George Lugomela alisema kwa wastani wingi wa maji yanayoingia katika bwawa la Mtera kipindi cha kiangazi ni mita za ujazo 1,470,000 kwa siku sawa na hifadhi mita za ujazo milioni 220.5.
Aidha, alisema wastani wa maji yanayohitajika katika jiji la Dodoma ni mita za ujazo milioni 130 kwa siku sawa na hifadhi mita za ujazo milioni 19.5.