‘Bwawa la Nyerere lilizuia Mafuriko Rufiji’

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema mradi wa Bwawa la Julius Nyerere lilizuia mafuriko wilayani Rufiji kwa zaidi ya miezi mitano katika kipindi cha mvua za El nino.

Amesema lengo la kuanzishwa kwa mradi huo lilikuwa kupunguza mafuriko na kufua umeme, malengo ambayo kwa kiasi kikubwa yametimia.

Matinyi amesema tangu kuanza kwa mvua za El nino mwezi Oktoba, bwawa hilo lilikuwa likihifadhi maji mengi yaliyokuwa yakipita katika Mto Rufiji hadi lilipojaa Machi 5, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 12, jijini Dar es Salaam, amesema baada ya kuanza kuhifadhi maji uwezekano wa mafuriko ulipungua.

Amesema bwawa hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 1194 lina uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo bilioni 32.7 ambapo lilianza kujaza maji Desemba 22, 2022 na lilitarajiwa kujaa kwa miaka mitatu.

“Kama tusingekuwa na hili bwawa mafuriko yangeanza kutusumbua eneo la la bonde la Mto Rufiji tangu mwezi Oktoba mwaka jana, bwawa hili lilituvusha hadi hapo lilipofikia ukomo.

“Kwa kuwa mvua ziliendelela na maji yakawa mengi Tanesco ilitaarifu mamalaka na wananchi walipewa taarifa ila hawakupenda kuondoka wakisema wameshazoea kukaa na maji,” amesema Matinyi.

Amesema kwa kuwa bwawa hilo lilifikia ukomo wa kuchukua maji, ilibidi maji yaendelee kupita katika mkondo wake wa kawaida na kusababisha hali ilyotokea, huku akisema uwepo wake ulizuia mafuriko na sio kusababisha mafuriko.

Habari Zifananazo

Back to top button