CAG abaini hasara bil 162/- mamlaka za maji

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini hasara ya Sh bilioni 162.2 inayotokana na ongezeko la kiwango cha upotevu wa maji kwa mamlaka 23 za maji na usafi wa mazingira.
Ametaja sababu zinazochangia upotevu wa maji ni pamoja na uchakavu wa miundombinu ya zamani inayosababisha uvujaji wa maji; na uunganishaji haramu unaosababisha kupotea kwa mapato.
Amesisitiza kuwa usiposhughulikiwa ipasavyo, mamlaka zitaendelea kupata hasara zisizo za lazima.
Wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeweka kiwango cha upotevu wa maji kinachokubalika kuwa kisizidi asilimia 20, ukaguzi wa CAG umebaini kwa miaka minne mfululizo, kiwango cha upotevu kwa mamlaka hizo 23 kinazidi asilimia 20.
Haya yamo katika ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
“Napendekeza serikali iendelee kuingilia kati kwa kupitia upya miundombinu ya usimamizi wa maji katika mamlaka za maji na kuandaa mipango ya kuboresha miundombinu hiyo kwa ajili ya kupunguza upotevu wa maji,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.
Mwenendo wa upotevu wa maji kulingana na ripoti za ukaguzi za mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira, unaonesha mamlaka hizo na kiwango cha upotevu kwa mwaka 2021/22 kwa asilimia katika mabano ni Bukoba (43), Morogoro (40), Musoma (39.90), Dar es Salaam (39.03), Njombe (39), Korogwe (38), Arusha (37), Mwanza (36), Lindi (35.20), Dodoma (33.6) na Tabora (31.84).
Mamlaka nyingine Sumbawanga, Tanga (30.70), Kigoma (30), Mtwara (29.13), Singida (29), Mbeya (28), Bariadi (27.50), Moshi (27.35), Babati (25.20), Shinyanga (24), Iringa (23) na Kahama ni asilimia 23.
Kwa mujibu wa CAG, upotevu wa maji ni kipimo muhimu cha ufanisi na utendaji wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira kwa kutathmini kiasi cha maji kinachozalishwa au kununuliwa lakini hupotea kabla ya kufikia wateja.
Upotevu wa maji huwasilishwa kwa asilimia na hutathminiwa kwa kutoa kiasi cha maji kilichouzwa kwa watumiaji kutoka kwenye jumla ya kiasi kilichozalishwa au kununuliwa.
Katika hatua nyingine, CAG amebaini upungufu katika usimamizi na udhibiti wa miundombinu ya maji.
Amependekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) itekeleze mpango wa kina na madhubuti wa udhibiti wa kutu na kuhakikisha mabomba yote ya chuma ya usambazaji na usafirishaji wa maji yanakingwa dhidi ya kutu.
Katika kutembelea mitambo ya uzalishaji maji ya Dawasa iliyopo Ruvu mkoani Pwani, alibaini kuwa mabomba yote yaliyopo chini hayakuwa yametengenezwa kuzuia kutu.
Alibaini pia bomba kuu la kupeleka maji Dar es Salaam kutoka katika chanzo cha Ruvu Chini na moja kutoka Ruvu Juu hayakuwa yametengenezwa kuzuia kutu.
Alisema uharibifu unaotokana na kutu katika mabomba unaweza kuhatarisha ubora wa maji na usalama, kusababisha uharibifu wa vifaa na kuongezeka gharama za matengenezo na hivyo kuongezeka kwa upotevu wa maji, kupungua kwa ufanisi wa usambazaji na kusababisha kuharibika kwa vifaa na kusimamisha huduma ya upatikanaji wa maji.