CAG abaini hitilafu makubaliano ya kukiri kosa

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka na maafisa wake walikiuka taratibu za makubaliano ya kukiri kosa katika kukamata, kuendesha mashtaka, na kushughulikia kesi.

Katika ripoti yake aliyoitoa jana kwa umma ya mwaka 2021/22, alisema ukiukwaji huo unaonesha ukosefu wa uwazi katika uandikishaji mikataba ya kukiri kosa, ambao unahitaji uchunguzi zaidi wa uwezekano wa uwepo wa ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya mamlaka.

Alisema katika ukaguzi maalumu kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mikataba ya Makubaliano ya kukiri kosa iliyosimamiwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilibainika washitakiwa wa makubaliano ya kukiri kosa hawajafanya malipo ya fidia ya Sh bilioni 170.61 kama ilivyokubalika katika makubaliano ya kukiri kosa na hukumu za Mahakama.

Alisema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alishindwa kukusanya ahadi hizo na hakuchukua hatua za kuwasilisha maombi ya kukamata mali kwa wale walioshindwa kutekeleza makubaliano ya ahadi.

Kichere alisema ukaguzi wake alibaini kuwa DPP alikusanya Sh bilioni 10.16 ambazo hazikuwa na uhusiano na mchakato wa kesi za kukiri kosa.

Alisema ukaguzi ulibaini kasoro katika taratibu za kufuatilia mali na fedha zilizotaifishwa, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa daftari sahihi la kurekodi fedha na mali zilizotaifishwa.

“Kasoro hizi zilisababisha athari mbaya, kama ile kupungua kwa thamani ya mali zilizotaifishwa na hasara ya kifedha kutokana na mali zilizosahaulika.”

Kichere pia alisema ukosefu wa taarifa za msingi za mali zilizotaifishwa baada ya uamuzi wa Mahakama, kunaonesha mapungufu katika usimamizi na ufuatiliaji wa mali zilizotaifishwa na ukaguzi ulibaini mapungufu katika usajili na umiliki wa magari yaliyotaifishwa na kutofanyika kwa tathmini ya mali zilizotaifishwa.

“Kulikuwa na mashaka juu ya usimamizi sahihi wa fedha zilizotaifishwa kutokana na kushindwa kurejeshwa kwa kiasi kikubwa cha fedha zilizotaifishwa kutoka kwenye mabenki ya biashara yaliyopo ndani na nje ya nchi. Kwa ujumla, ukaguzi umebaini haja ya uwepo wa taratibu bora za ufuatiliaji na usimamizi wa mali na fedha zilizotaifishwa.”

Habari Zifananazo

Back to top button