CAG apendekeza tathmini manufaa bei za mazao

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amependekeza serikali ifanye tathmini kuhakiki kama kuongezeka kwa bei za mazao ya chakula kunawanufaisha wakulima ama hakuwanufaishi na kuchukua hatua stahiki kutokana na matokeo ya tathmini itakayofanyika.

Mapendekezo hayo yamo kwenye Ripoti ya CAG ya ukaguzi wa mashirika na taasisi za serikali wa mwaka 2021/2022 ukiwamo ukaguzi wa bodi za mazao.

Katika Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, CAG amebaini kuna changamoto ya kushindwa kufanya biashara ya nafaka na mazao mengine kwa ushindani.

Kuhusu manufaa kwa mkulima, amependekeza ifanyike tathmini kwa kuwa hakuna ushahidi wa tathmini unaoonesha kwamba kupanda kwa bei ya mazao ya chakula kunawanufaisha wakulima wa mazao husika.

CAG ameeleza kuwa kuna hatari na uwezekano kuwa kupanda kwa bei ya mazao ya chakula hakuwanufaishi wakulima ila kunawaathiri kwa kuwa wengi ni wadogo na wanafanya kilimo cha kujikimu hivyo hawana uwezo wa kuhifadhi mazao ili kuuza baadaye bei zikiwa zimepanda.

Kwa mujibu wa CAG, ripoti zake za miaka ya nyuma zimekuwa zikieleza kuwa mazao ya vyakula na mazao mengine yamekuwa yakikabiliwa na kukosekana kwa masoko ya uhakika hivyo kusababisha wakulima wauze mazao kwa bei ndogo.

Ameeleza kuwa serikali imechukua hatua kukabili changamoto ya kukosekana kwa masoko ya uhakika hasa mazao ya chakula na mazao mengine.

“Kwa mfano, baada ya serikali kufanya tathmini ya utoshelevu wa chakula nchini, ilifungua mipaka ya nchi kwa wafanyabiashara wa nje kuja kununua mazao kutoka soko la ndani la Tanzania na kusafirisha nje ya nchi,” ameeleza CAG.

Wakati huohuo, ripoti hiyo imeeleza kuwa wakati wa ukaguzi wa CAG kwa bodi za mazao na majukumu ya bodi hizo imebainika Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeshindwa kufanya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko kwa ushindani na kwa ufanisi.

Ripoti inaeleza kuwa bodi ilianzishwa ili kuwapa wakulima soko la uhakika la nafaka na mazao mchanganyiko na kuongeza uuzaji wa mazao hayo nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni.

Majukumu ya msingi ya bodi ni pamoja na kufanya biashara itakayowezesha ukuaji wa sekta ya kilimo cha nafaka na mazao mengine.

Hata hivyo, CAG amebaini bodi ina changamoto ya kushindwa kufanya biashara ya nafaka na mazao mengine kwa ushindani nchini.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alibaini kuwa mbinu na mikakati ya kibiashara inayotumiwa na Bodi haina ufanisi wa kutosha kwa kuwa inafanya kazi chini ya uwezo wake na haifanyi tathmini ya kurejesha gharama zote za uendeshaji.

Habari Zifananazo

Back to top button