Casemiro, Fred wajiangalie leo
Endapo wachezaji Carlos Casemiro na Frederico Santos ‘Fred’ wataoneshwa kadi za njano katika mchezo wa leo wa EPL dhidi ya Crystal Palace, watakosa mchezo wa Jumapili dhidi ya Arsenal katika Uwanja wa Emirates.
Kanuni za EPL zinasema mchezaji atakayepata kadi tano za njano katika michezo 19 iliyopita , atafungiwa mchezo mmoja.
Kabla ya mchezo dhidi ya Manchester City uliopigwa Jumamosi iliyopita, wachezaji hao walikuwa na kadi tatu za njano, katika mchezo huo ambao Man United ilipata ushindi wa mabao 2-1, Fred na Casemiro walipata kadi za njano na kuwa kadi nne.
Katika mchezo wa leo dhidi ya Palace, mmoja wao au wote wakipata kadi ya njano itakuwa kadi ya tano hivyo watakosekana katika mchezo dhidi ya Arsenal.
Manchester United inaingia katika mchezo huo ikiwa nafasi ya nne na pointi 38, wakati Palace inayoshika nafasi ya 12 ikiwa na pointi 22 katika msimamo wa Ligi Kuu England.