CCM Dar es Salaam wakutana kuchagua Mwenyekiti

Nani Kuongoza CCM Dar es Salaam

UCHAGUZI wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam unaendelea ambapo wagombea, Mama Kate Kamba anatetea nafasi hiyo dhidi ya wagombea wengine watatu.

Katika orodha ya wateule, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mstaafu wa Jeshi la Polisi nchini SACP Jamal Rwambow, mwanasiasa na Mbunge wa zamani wa Temeke Abbas Mtemvu na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga wanawani kiti hicho.

Uchaguzi huu ni muhimu kwa CCM kuelekea maandalizi ya Uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025. Akiomba kura, Abbas Mtemvu amesema anatambua jukumu la 2024 na kwamba akipewa idhini chama “hakitajutia.”

Advertisement

Mwenyekiti wa CCM anayemaliza muda wake wa miaka mitano, Kate Kamba amesema wanachama wa CCM wanafahamu kazi iliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano na kwamba “mnanifahamu vizuri,” amesema akiomba kura kwa wajumbe wa mkutano huo unaofanyika ukumbi wa Mawela, Sinza jijini Dar es Salaam.

Baraka Konisaga, kada wa CCM ambaye amekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu kwa miaka 20 mfululizo amesema anaomba nafasi ya uongozi ili akishukuru chama chake.

 

“Nimestaafu nikaangalia nafasi yangu na chama changu kinapoenda. Tuna Ligi 2025 nikajiuliza ni kapteni gani katika usajili atakayeongeza ushindi mkuu 2025? Kocha mahiri akiwa Samia Suluhu Hassan, basi naomba kura zenu hamtapoteza mwelekeo 2025,” amesema.

Wakati Dar es Salaam wanakutana kuamua nani atakuwa kiongozi wao kwa mkoa, CCM imefuta matokeo ya uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti Umoja wa Vijana Mkoa wa Simiyu na kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho katika mikoa ya Mbeya na Arusha.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amewaambia waandishi wa Habari mjini Dodoma leo Novemba 21 kuwa maamuzi hayo yametokana na dosari katika mchakato wa uchaguzi sambamba na tuhuma za rushwa.

Haikufahamika ni lini uchaguzi wa Mwenyekiti UVCCM Simiyu utarudiwa ama maamuzi ya mwisho kuhusu mchakato wa uchaguzi Mkoa wa Mbeya na Arusha yatafanyika.

Mama Kate Kamba

Habarileo inafahamu kuwa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa umepangwa kufanyika Novemba 24 jijini Dodoma ambapo wajumbe 893 wamepangwa kuhudhuria. 

Mkutano huo wa siku mbili unalenga pamoja na mambo mengine kufanya uchaguzi wa viongozi wa jumuiya ngazi ya taifa. Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Gilbert Kalima amesema nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe watano wa NEC ya CCM. Pia kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe sita wa Baraza Kuu la Wazazi taifa.

Wagombea waliopitishwa na vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi wanatarajiwa kuwasili jijini Dodoma leo Novemba 21 kujiandaa na uchaguzi huo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *