Kinana: CCM ina taratibu zake

KAGERA: MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema CCM inataratibu zake za kupata viongozi na mchakato wa ndani ya chama hicho utaanza Julai 2025.

Aidha, amewaonya wanachama wa chama hicho kuacha kupoteza muda wa kupanga safu hivi sasa na badala yake waelekeze nguvu katika kutekeleza ilani ya CCM kwakupeleka maendeleo kwa wananchi.

Advertisement

Kinana ameyasema hayo leo wakati akiagana na wazee wa Mkoa wa Kagera katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kagera, akielekea wilayani Chato.

Amesema, “niwaombe mshikamane kuwaletea wananchi maendeleo, msihangaike sasa hivi na nani achukue nafasi ipi, mnapoteza muda mwingi tumtoe huyu, tumtoe yule, mnamzungumzia Mbunge, Mbunge si yupo na CCM inataratibu zake 2025 itajulikana, ” amesisitiza Kinana.

Amesema, wana CCM wanapaswa kushughulika na shida za wananchi kwani ndio watakaowahoji mliahidi hiki na kile kiko wapi?

“Tujipange, usipojipanga utapangwa, sisi sio chama tawala sisi ni chama cha siasa, ile kauli ya CCM chama dume kigumu kutoka madarakani, hiki ni Chama cha Demokrasia, tusing’ang’ane na kushika Dola, Dola watu wakifanyiwa vizuri watawachagua tu.

“Mara nyingi ni rahisi kusema, kutenda ngumu, tushikamane tuna kazi ngumu mbele yetu,” amesema Kinana

Aidha, Kinana amekemea tabia ya usaliti kwa baadhi ya wana CCM.

“Hakuna mahali CCM imeshindwa, iliposhindwa kote sio upinzani ni mamluki, tulifanya tathimini majimbo yote yaliyochukuliwa na upinzani wakati ule mchango mkubwa ulitokana na nguo za kijani Iyena iyena.

“Wananchi watatuamini tukiwafanyia kazi nzuri, “amesisitiza Kinana.

11 comments

Comments are closed.