WAJUMBE wanne wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, wakiongozwa na Salim Asas wamefanya mashambulizi ya kisiasa katika mkutano wa kwanza wa hadhara wa chama hicho mkoani Iringa uliofanyika katika kijiji cha Kiyowela, kata ya Kiyowela wilayani Mufindi.
Wengine walioshiriki mkutano huo mkubwa uliokwenda sambamba na uzinduzi wa sherehe za miaka 46 ya CCM ni pamoja na Richard Kasesela, Leonard Mahenda (Qwihaya) na George Gandye ambao wote ni wakazi wa Iringa.
Pia alikuwepo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ambaye kwa nafasi yake kama mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa ya chama hicho alitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani tangu serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan iingie madarakani.
Kwa upande wake, Asas alisema CCM ni chama cha vitendo, kinaahidi na kutekeleza na kwa kupitia mikutano watakayoendelea kuifanya watajikita katika kuuelezea umma nini serikali yao imefanya, inaendelea kufanya na itafanya kwa maendeleo ya wananchi na Taifa.
“Maendeleo ni mchakato na ni mahitaji yanayoongezeka kila siku kutokana na ongezeko la watu. Kwa hiyo tunaahidi, tunatekeleza na tunaboresha kwa kuzingatia mahitaji hayo,” alisema.
Akizindua ofisi ya CCM ya kata hiyo inayojengwa kwa ufadhili wake wa zaidi ya Sh Milioni 52, aliahidi pia kuchangia ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari Kiyowela ili kuwanusuru wanafunzi wa kike wanaotembea zaidi ya kilometa saba kwenda shuleni.
Awali Diwani wa Kata ya Kiyowela, Steven Muhumba alisema katika mkutano huo kwamba ukosefu wa bweni katika shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 400 unawaweka wanafunzi hasa wasichana katika mazingira hatarishi na akaomba msaada wa ujenzi wa bweni litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 200.
Kwa upande wake Qwihaya aliahidi kuchangia tripu 20 za tofari kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo huku Mkuu wa Mkoa akisema serikali itaweka pia mkono wake katika shughuli hiyo.
“Qwihaya ameahidi tripu 20 na serikali ya mkoa imesema itaweka mkono wake; mimi naahidi sehemu yote itakayobaki katika ujenzi wa bweni hilo, nitaikamilisha,” Asas alisema na kuamsha vigelegele kutoka kwa wananchi.
Wakati Mnec Gandye akiwataka wananchi kuimba wimbo wa ‘Samia Tena’ kama wanataka kuendelea kukua kiuchumi, Kasesela kwa upande wake aliwaomba wapinzani kutosimamisha mgombea wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 na badala yake kiti hicho wamuachie Dk Samia.
“Toka wapinzani waanze mikutano yao mmewasikia pia wanavyomfagilia Rais Mama Samia kwa jinsi anavyoupiga mwingi. Ili heshima hiyo wanayompa iwe ya kweli, basi tuwaombe wamuache mama apite bila kupingwa, wao waje huku kwenye ubunge na udiwani tuchuane,” alisema Kasesela..