MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho mkoani humo kuepuka majungu, badala yake watengeneze uhusiano mzuri na watumishi kwa kuwa wao ndio watekelezaji wa Ilani.
Kimanta ametoa kauli hiyo akiwa Kijiji cha Mpembe, Kitongoji cha Kabatini Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, wakati akihutubia wananchi wa kitongoji hicho kelele cha maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa chama hicho.
Amesema kamati ya siasa mkoani humo haitasita kumchukulia hatua kiongozi wa chama ambaye atabainika kuvuruga uhusiano baina ya serikali na chama, pia tumishi atakayebainika kuvuruga uhusiano baina ya chama na serikali.
“Sisi wote ni binadamu, kukitokea kutoelewana basi kutoelewana huko kuzungumzwe kwa kuheshimiana, hatutarajii tufike mahali tukute kiongozi wa chama au kiongozi wa serikali anamdharau mwenzake,” amesema.
Ametoa wito kwa wana CCM kutambua wajibu wao, kufanya ziara kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua, huku akiwasihii Watanzania kuendelea kuwa na imani na chama cha mapinduzi kwa kuwa ndicho chama pekee kinachoweza kutatua kero zao.