CCM kuwaweka kitimoto mawaziri watano

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuanzia Jumatatu ijayo kitawaweka kitimoto mawaziri wa sekta tano wajibu kero za wananchi wa mikoa ya Singida na Manyara.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alizitaja sekta hizo ni maji, ujenzi na uchukuzi, maliasili na utalii, afya na kilimo.

Chongolo amesema Jumatatu wiki ijayo ataanza kuwaita mawaziri wa wizara husika ikiwemo ya maji kwa kuwa wananchi wamelalamika kukosa maji safi. Alisema pia wananchi wamelalamika ubovu wa barabara ya Arusha-Kiteto-Kongwa.

Advertisement

Aidha, Chongolo alisema kero ya chakula cha njaa, uhaba wa vituo vya afya, dawa na vifaa tiba na kero nyingine zilizoibuliwa na wananchi na zinahitaji majibu.

“Nimepita mikoa mingi kero ni nyingi, wananchi wanapata taabu waliopewa mamlaka baadhi hawashuki chini kuyatatua, sasa wiki ijayo nitaanza na mawaziri wa sekta hizo nitakutana nao wanipe majibu,” alisema

Jana wakati akiwa njiani kutoka wilayani Simanjiro kwenda Kiteto, msafara wa Chongolo ulisimamishwa na wananchi wa Kata na Kijiji cha Ndaleta na wakalalamika kuhusu wanyama hasa tembo kuharibu mazao shambani.

Mwakilishi wa wananchi hao, Ijumaa Bakari alisema wamechoshwa na tembo wanaovamia maeneo yao kutoka Hifadhi ya Indema iliyo chini ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) wilayani Kiteto mkoani Manyara.

Alisema mwaka 2021, kijiji kilifanya tathmini ya kulipa fidia uharibifu uliofanywa na tembo na majina ya wananchi ambao mashamba yao yaliharibiwa yalikwenda kwenye mamlaka husika na mwaka jana yalirudi na wakatakiwa wapeleke namba za Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili fedha zitolewe ila hadi sasa hakuna lililofanyika na tembo bado ni kero.

Walitaja changamoto nyingine katika hifadhi hiyo ni manyanyaso ya wananchi kupigwa na kunyang’anywa mashamba licha ya viongozi wa mkoa kuwaruhusu kufanya shughuli za kilimo.

Alisema ni miaka zaidi ya tisa sasa hawafanyi shughuli za kilimo katika maeneo yao, hivyo wanashindwa kuzalisha na kupata fedha za kuwasomesha na kuinua kipato cha familia zao.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere alikiri kuwapo na kero hiyo ya tembo na kuna shule ya sekondari katika eneo hilo tembo wanaingia mpaka kwenye mabweni.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, aliwasihi wananchi waendelee kukiamini chama kwa sababu kitashughulikia kero zao.