CCM: Msimchezee Simba Sharubu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan hakuna mbadhilifu wala muhujumu miradi ya maendeleo ambae atavumiliwa.

Akizungumza leo Novemba 5,2022 kwenye ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar Es Salaam katika Kongamano maalum la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa Taifa ikiwemo kufungua matumaini mapya, furaha na mwanga wa maendeleo kwa wananchi, Katibu wa wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema wapo baadhi ya watendaji wa Serikali walioaminiwa na kupewa dhamana sio waadilifu.

“Nataka niwaambie wale wote walioaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wachunge dhamana zao, wapo wanaodhani pochi la mama lipo wazi, kuna mianya ya upigaji basi wanachota tu fedha, nawaambia, Simba ni Simba tu, na Simba hachezewi sharubu.”Amesema Shaka na kuongeza

“Yeyote atakae hujumu fedha za miradi ya maendeleo, mla rushwa, mbadhilifu, mpigaji, kwenye utawala huu wajue wanacheza na moto, Rais hatokua na simile kuwavumilia.” Amesema

Aidha, Shaka amesema chini ya uongozi wa Rais Samia umefungua nchi na kuleta mwanga mpya wa matumaini

“Lengo kuu la Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ni kumkomboa mwananchi kutoka katika wimbi la umasikini. Katika kipindi chake cha mwaka mmoja na miezi minane tunampogeza Rais Samia kwa kuimarisha Demokrasia yetu kwa mataifa jirani na mataifa ya nje katika sekta za kiuchumi na kisiasa.” Amesema na kuongezea

“Rais Samia amezitembelea nchi takribani 22 kwa zaidi ya awamu 25 nchi yetu imeendelea kufunguka kiuchumi kupitia biashara na nchi za nje. Takwimu za hivi karibuni zimerekodi ongezeko kubwa la mauzo ya nje kwa bidhaa na huduma za Tanzania katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.” Amesema.

Amesema takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya nchini Kenya (Kenya National Bureau of Statistics) zimeonesha kukua maradufu kwa mauzo ya Tanzania katika nchi hiyo kwa takribani shilingi bilioni 20.5 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2021/2022 kutoka shilingj bilioni 10.8 kwa mwaka uliopita wa 2020/2021.

“Nitumie fursa hii pia kumpongeza Rais Samia kwa ziara yake ya China ambayo imeitimishwa jana Novemba 4, 2022. Tumeshudia mikataba ya ushirikiano ikisainiwa kuna mikataba ya ushirikiano biashara, uwekezaji, uchumi wa kidigitali, ushirikiano katika maendeleo, masuala ya mazingira, uchumi wa bluu na kubadilishana uzoefu katika nyanja ya sayansi na teknolojia,”amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button