CCM: Muungano utaendelea kuwa mfano Afrika

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema serikali yake itaendelea kudumisha utambulisho wa Watanzania kwa kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taarifa ya Ubalozi wa Tanzania nchini China kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, imeeleza kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amesema hayo jijini Guangzhou nchini China katika hafla ya kuadhimisha miaka 59 ya Muungano.
“Muungano huo utaendelea kuwa mfano wa kuigwa na nchi za Afrika, kuwa bara letu linaweza kuungana na kuwa kitu kimoja,” alisema Chongolo.
Aliongeza: “Tunaposherehekea miaka 59 ya Muungano wetu, hatuna budi kutilia maanani kuwa Tanzania si kisiwa na hivyo ustawi wetu unategemea pia mazingira ya kimataifa. Kwa ujumla mazingira ya kimataifa hayajakuwa na unafuu mkubwa katika kipindi hiki.”
Aliishukuru Serikali ya China kwa kuungana na Tanzania katika safari ya Muungano iliyoanza miaka 59 iliyopita ambayo pia ni miaka 59 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi hizo.
“Tunashukuru kwa kutuunga mkono, kututia moyo na kutusaidia tulipohitaji msaada wenu. Tunathamini sana michango yenu yote ya fedha, hali na mali. Mmetuhakikishia urafiki wa kweli na tunapenda kuendelea kushirikiana nanyi katika kipindi kijacho chini ya hadhi mpya ya ushirikiano wetu,” alisema Chongolo.
Aliahidi Tanzania itaendelea kuenzi, kuheshimu na kuimarisha ushirikiano na China katika nyanja za siasa baina ya CCM na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).
Pia Chongolo alisema Tanzania itaendelea kuenzi na kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na Serikali ya China na baina ya majeshi ya nchi hizo.
Alihimiza Watanzania wanaoishi China wawe waaminifu kwa wenzao waliopo nyumbani.
“Wenzako wanapokutuma kazi ya kuwatafutia mahitaji hakikisha unaifanya kwa weledi na uaminifu…na msitumie ‘advantage’ ya wenzenu kutofahamu gharama za vitu kuwalalia kwa bei za juu,” alisema Chongolo.
Pia alitoa mwito kwa Watanzania nchini humo washirikiane kuongeza nguvu ya kunufaika na fursa zilizopo China.
“Waswahili wanasema kidole kimoja hakivunji chawa. Lazima kushikamana na kushirikiana ili kunufaika. Hapa kuna fursa kwa kila mmoja. Tusiweke mbele ubinafsi, umimi na roho ya kwanini apate,” alisema Chongolo.
Alitoa mwito kwa Watanzania nchini humo waongeze jitihada za kuvutia teknolojia na mitaji sanjari na kuchangamkia masoko ya bidhaa.