CCM: Ni bajeti ya wananchi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza Serikali kwa kuwasilisha Bajeti yake  kwa mwaka 2023/24 ambayo imegusa mwananchi moja kwa moja kwa kufungua fursa za kiuchumi na kuweka uwekezaji mazingira rafiki ya kibishara.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kingiti, Kata ya Kingiti, Wilaya ya Mpwapwa mkoani hapa jana, Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, alisema sura ya bejeti imebeba dhamira ya dhati ya serikali ya kujenga uchumi wa nchi ambao uliteteleka kutokana na ugonjwa wa Covid 19 na vita ya Ukraine na Urusi.

Chongolo alisema CCM inaipongeza serikali kwa bajeti nzuri kwani inakwenda kugusa maisha ya wananchi wa kawaida.

Advertisement

Alisema, malengo na makusudio ya bajeti hiyo kwanza ni kujielekeza katika kulinda viwanda vya ndani suala ambalo ni msingi kwa maendeleo ya nchi yeyote duniani.

“Uchumi wa nchi unaimarika kwa namna tunavyotoa bidhaa kwenda nje zaidi na tunavyoleta fedha za kigeni. Viwanda vikitengenezwa hapa tukitoa bidhaa tukapeleka Zambia, Congo maana yake tunaongeza fedha za kigeni na hayo ni maendeleo yenyewe.”

Aidha, Chongolo alisema baadhi ya maeneo muhimu ambayo bajeti hiyo imegusa ni pamoja na suala la utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati uamuzi ambao utachochea upatikanaji wa wataalamu wa ngazi ya kati.

“Hilo ni jambo kubwa na lamaana, zamani tulikuwa tunaweka msukumo kupeleka vijana chuo kikuu, kwa sababu hiyo tabaka la mafundi mchundo likawa linakufa na likafa kwa kiwango kikubwa. Ukiangalia kazi nyingi za kitaalamu zinafanywa na mafundi wa kati..”

Chongolo alisema uamuzi huo wa serikali una lengo la kuwajenga vijana wenye uwezo wa kujitegemea zaidi kuliko wanaosubiri kuajiriwa.

Alisema, eneo lingine ambalo linagusa wananchi ni kuondolewa kwa tozo kwenye simu ambako pia alisema kutaongeza fursa kwa watu kutumia simu zaidi.

Chongolo alisema eneo lingine ni zuio la biashara na kuwa hatuan hiyo imegusia wananchi kwa kuweka mkazo kwamba hakuna sababu ya kufungwa biashara kwa suala ambalo linaweza kujadiliwa.

“Siku za hivi karibuni kulitokea wimbi la watu kila akiamka asubuhi anaamua kwenda kufunga biashara ya mtu, mtu unatakiwa kufanya biashara ili kupata fedha kulipia hicho kitu anachodaiwa, lakini mtu anakwenda kufunga biashara sasa utakwenda kupata wapi pesa.”

Kwa upande wa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alisema bajeti ya serikali inakwenda kumkomboa mwanamke wa kitanzania hasa kutokana na kiasi kikubwa takribani trilioni 1 zinaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maji.

/* */