CCM ‘ni Dk Samia’

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM wamemchugua Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kura 1,914 kati ya 1915, kuwa Mwenyekiti CCM kwa miaka mitano tangu 2022 hadi 2027.

Matokeo hayo yanaonesha kwamba ni kura moja tu ya hapana lakini hakuna kura iliyoharibika.

Akitangaza Matokeo ya Uchaguzi wa Viongozi wa Juu wa CCM katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Muda Dk Mohammed Ali Shein  alisema kwa ushindi huo wa kura anamtangaza Dk Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Pia Dk Shein alimtangaza mrithi wake Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar baada ya kupata kura 1912 kati ya 1,915 zilizopigwa.

Dk Hussein Mwinyi ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anachukua nafasi hiyo baada ya Dk Shein kumaliza muda wake. Dk Mwinyi alipata kura za hapana tatu.

Katika uchaguzi huo pia alimtangaza Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Komrade Abdurahman Kinana kwa kupata kura 1,913 kati ya 1,915.

Kinana amepata kura za hapana mbili.

Pia Dk Shein aliwatangaza washindi wa nafasi 40 za Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ambao kati ya 20 wanatoka Zanzibar wakiwemo wanaume 14 na wanawake sita na vilevile wajumbe 20 kutoka Bara wakiwemo wanaume 14 na wanawake sita.

Katika uchaguzi wa wajumbe wa NEC walikuwa katika mnyukano mkali lakini baadhi ya majina ya mawaziri, wabunge na watendaji serikalini waliokuwa wakitajwa sana wameshindwa kupenya na huku sura mpya ziking’ara ambazo Ilikuwa zikipewa nafasi ndogo katika pande zote mbili za Muungano Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kiti, Mwenyekiti wa Chama Dk Samia aliwapongeza wajumbe kwa kuchagua yeye na viongozi wenzake katika chama.

Pia alimpongeza mwenyekiti wa muda Dk Shein kwa kuendesha uchaguzi vizuri pamoja na kamati ya uchaguzi pamoja na wasaidizi wao kwani wakati wanapanga ratiba walijua wangekesha.

Habari Zifananazo

Back to top button