CCM yaazimia mambo 3 uwekezaji bandari

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maazimio matatu katika uwekezaji na uendeshaji wa bandari. Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ilikutana jijini Dodoma jana katika kikao cha kawaida kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mapema jana. Katibu wa Halmashauri Mkuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alisema hayo usiku alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kikao cha kawaida cha NEC taifa.

Mjema alisema Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilipokea na kujadili taarifa ya makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari na kuazimia mambo matatu.

Alisema NEC ya CCM imeazimia kuwa uwekezaji na uendeshaji wa bandari ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi. Mjema alisema pia imekubaliana kuwa uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, ibara ya 59, ukurasa wa 92.

Alisema pia NEC ya CCM imeazimia kuwa serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari. Aidha, Mjema alisema pia Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kauli moja imezipongeza serikali zote mbili za CCM kwa kuendelea kutafsiri kwa vitendo ilani kwa maslahi na ustawi wa Watanzania.

“NEC Taifa imezipongeza Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutafsiri kwa vitendo llani ya CCM ya Mwaka 2020- 2025, kwa maslahi na ustawi wa Watanzania wote,” alisema.

Hivi karibuni Bunge lilipitisha azimio la ushirikiano kati ya Serikali ya Dubai na Tanzania kwenye eneo la bandari. Juni 28 mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifunga Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 jijini Dodoma alisema serikali itachukua maoni na ushauri uliotolewa na wananchi kuhusu suala hilo.

“Ninachoahidi ni kwamba maoni na ushauri huo tutakwenda kuyatumia kwenye mikataba mahususi ya uwekezaji tutakayokwenda kuingia na wenzetu. “Kilichofanyika sasa ni kwa Bunge kuridhia ushirikiano baina ya nchi mbili kama sheria zetu zinavyotaka,” alisema Majaliwa.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button