CCM yadai CHADEMA imepokea ruzuku walioisusia

DAR ES SALAAM: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuweka wazi kuwa kimeshalipwa Sh bilioni 2.7 ya ruzuku.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana akizungumza na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee amesema CHADEMA katika kikao cha maridhiano walikuwa na utitiri wa hoja na moja ya masharti ambayo walitoa katika maridhiano hayo ni kulipwa ruzuku yao ya miaka mitatu Sh bilioni 2.7.

CHADEMA walizidai fedha hizo ambazo walisusia kwa madai ya uchaguzi uliopita wa mwaka 2020 kuvurugwa kwa lengo la kupendelea upande mmoja wa siasa.

Chadema pia walikosoa vikali kitendo cha waliokuwa wanachama wake 19 wanawake kuingizwa bungeni kinyemela bila ridhaa ya chama.

Akizungumza Kinana amesema “Walikuja na hoja ohoo sisi tangu uchaguzi umekwisha hatujachukua ruzuku kwa kuwa tumezungumza na tumeanza kuelewana tulipeni ruzuku yetu ya miaka mitatu, ruzuku.

“Kwa kawaida, ruzukku inapitia kwenye bajeti ya serikali, ruzuku yako ikishapita imepita, sasa wao wanataka ruzuku ya mwaka 2021, 2022, 2023 nikawahoji si mlikataa wenyewe, wakasema haa! si tunazungumza maridhiano tupeni hela zetu.

“Nikaenda kwa Rais Samia na kumjulisha kuwa wanadai hela zao, Rais akasema hizi hela si zangu ni hela za serikali ngoja niulize kwanza, alipouliza akambiwa Rais bajeti ya miaka mitatu imeshapita, fedha hizo hazipo, Rais akaniagiza niwaambie watazipata kuanzia za bajeti ya mwaka huo 2022, nikawajibu CHADEMA ili jambo gumu wakasema haliwezi kuwa gumu serikali si ni yenu ya Chama Cha Mapinduzi.

“Rais akawa muungwana akasema isiwe shari, akaagiza serikali itafute utaratibu wa kuwalipa ili wapate haki yao wanayodai kudhulumiwa, kwa nini walikataa kwa sababu hawakutambua matokeo, mkitupa hela itakuwa mwanzo mzuri wa kutambuana, tukasema hatuwapi fedha kwa sababu mtutambue, tunawapa kwa sababu tupo kwenye mazungumzo ya kiungwana ya maridhiano kwa hiyo wakalipwa Sh bilioni 2.7.

“Nataka tuwaulize watanzania wapi CHADEMA imewahi kusema serikali imewalipa fedha hizi za ruzuku?” amehoji Kinana.

Aidha Kinana amesema kuhusu hoja ya wabunge wao 19 kuwa hawapo kihalali bungeni lazima watoke, waliwagomea kwa kile walichoeleza kuwa kipo nje ya uwezo wao.

“Niwasifu wenzetu ni mabingwa wa kujieleza, walitueleza kwa kina kwa nini wanataka wabunge wao 19 watolewe bungeni, lakini wakati tunazungumza jambo hili lipo mahakamani, jambo hili Rais hawezi kuingilia kesi ikiwa mahakamani, wakasema hizi mbinu za CCM ili wabunge wabaki ndani, hii sio ya CCM kila mtu ana dai haki yake. Mahakama ni mahali pa haki tukawambia hili hatuna mamlaka nalo,”amesema Kinana.

Habari Zifananazo

Back to top button