CCM yaeleza sababu za kuwapongeza Samia, Mwinyi

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa imeeleza sababu tano za kumpongeza Rais Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi.

Akielezea maazimio ya kikao cha chama hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti chama hicho, Samia Suluhu Hassan jana, Septemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amesema kikao maalum kilichoongozwa na na kujadili taarifa kutoka vitengo vya chama kuhusu utekelezaji wa kazi za chama na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Shaka amesema baada ya kujadili kwa kina, kamati kuu imefikia uamuzi wa kumpongeza Rais Samia kwa namna anavyoendelea kuiongoza nchi na kutafsiri kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 –2025.

“Pia ameimarisha huduma za kijamii, kuimarisha ustawi wa wananchi, kukuza
uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja ikiwa ni kushamirisha na kuharakisha maendeleo endelevu,” alieleza.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Shaka, hatua ya Rais Samia kutoa kipaumbele katika maeneo muhimu ikiwemo sekta ya kilimo.

“Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/2023, imeweka msukumo mkubwa katika kuboresha kilimo kwa kutenga bajeti kiasi cha shilingi bilioni 954 ikiwa ni ongezeko la asilimia 224.”Amesema Shaka

Amesema fedha katika bajeti hiyo zimeelekezwa katika ruzuku ya mbolea kwa ajili ya kuongeza tija na kushusha bei ya pembejeo kwa wakulima pamoja na ujenzi wa
miundombinu ya umwagiliaji.

“Serikali imetambua kilimo cha kisasa kitaongeza ajira, kitaongeza kipato cha wakulima, kitaiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula, kitaimarisha uzalishaji na uchumi wa nchi,”amesema

Ameeleza kuwa Kamati Kuu ya CCM imempongeza kiongozi huyo wa nchi kwa kusimamia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo kwa mara ya kwanza limeendeshwa kidijitali hapa nchini.

Aidha, Shaka amesema kamati hiyo imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, DkHussein Ali Mwinyi kwa jinsi ambavyo ameendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kiuchumi na kijamii kwa mafanikio makubwa pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya rushwa, uhujumu uchumi na ufisadi.

Habari Zifananazo

Back to top button