CCM yaguswa ripoti za CAG, Takukuru

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imeipongeza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kufanya kazi kwa weledi na kuonesha maeneo yaliyoboreshwa na serikali.

Kamati pia ilipongeza taasisi hizo kwa kubainisha udhaifu na kutoa ushauri kwa maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwenye ripoti walizowasilisha ili kuondoa ubadhirifu wa mali za umma.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema alipozungumza na vyombo vya habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam jana. Mjema alisema pongezi hizo ni sehemu ya maazimio yaliyotolewa na kamati hiyo katika kikao cha kawaida kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Dk Samia Suluhu Hassan.

“Kamati ilikutana katika kikao cha kawaida chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, imezipongeza serikali zote mbili (Bara na Zanzibar) kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,” alisema.

Alisema ripoti hiyo imeonesha kuwa serikali imeweza kuboresha maeneo mengi kwa asilimia 99 katika kutekeleza maendeleo lakini pia imesikitishwa na maeneo yaliyoonesha udhaifu kutokana na ubadhirifu.

“Kamati imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa ikiwemo taarifa ya CAG na Takukuru 2021/2022 ambazo ziliwasilishwa na kubaini kuwa serikali imeendelea kuboresha huduma kwa wananchi ikiwemo udhibiti na umakini wa matumizi ambapo asilimia 99 imepata hati safi,” alisema.

Alisema hata hivyo yapo maeneo ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ikiwamo kuimarishwa mifumo ya ukusanyaji mapato na tatizo la mifumo kutosomana huku akiongeza kuwa hilo limesababishwa na kuwepo baadhi ya watendaji wasio waaminifu na kusababisha hasara kwa serikali.

Mjema alisema katika kikao hicho pamoja na mambo mengine kamati hiyo ilitoa maazimio kadhaa kwa ajili ya uboreshaji zaidi ikiwa ni pamoja na kuelekeza serikali ichukue hatua thabiti kwa wote waliohusika katika ukiukwaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali za wananchi.

Pia kamati ilitaka serikali iwafuatilie viongozi wanaotumia vibaya dhamana ya uongozi na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele, badala yake wanaweka maslahi binafsi mbele. Aidha, alisema kamati iliipongeza serikali kwa kuratibu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyefanya ziara ya siku tatu nchini ambayo ilielezwa kuwa itaimarisha uhusiano wa uchumi na diplomasia kwa nchi hizo mbili.

Habari Zifananazo

Back to top button