CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa masikitiko na huzuni taarifa za kifo cha Rais wa zamani wa China Jiang Zemin aliyefariki Jumatano 30, Novemba, 2022.
Katika salamu za rambirambi zilizotumwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara komredi Abdulrahman Kinana kwa niaba ya CCM amesema kuwa hayati Jiang alikuwa nguzo muhimu ya uongozi wa Taifa hilo na aliweka misingi imara ya kiuchumi, kidiplomasia, umoja na mshikamano.
“Komredi Jiang Zemin alikuwa ni mhimili muhimu katika kipindi chake cha uongozi, aliwaongoza wananchi wa China katika mageuzi ya kiuchumi na kufahamu umuhimu wa kuziunganisha Hong Kong na Macau katika Taifa lao mama la Jamhuri ya watu wa China.” Amesema Kinana
Amesema, hayati Jiang alikuwa chachu ya jukwaa la kihistoria la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
“Tutamkumbuka kwa miaka mingi ijayo kutokana na kujitoa kwake katika kusimamia maendeleo ya China, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.” Amesema
Amesema, CCM kimekuwa na mahusiano wa kindugu na kihistoria na Chama Cha kikomunisti Cha China (CPC) ambayo yameendelea kuimarishwa katika awamu zote za uongozi.