CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kukubali maridhiano.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda ametoa kauli hiyo Januari 22, 2024 wilayani Hai mkoani Kilimanjaro alipozungumza na wananchi katika muendelezo wa ziara yake ya mikoa 20 nchini.
“Yaani yule kaka yangu Mbowe, linapokuja suala la fedha na kuomba michango kwa viongozi wa serikali anakubali maridhiano, tunapokuja ajenda za umoja wa kitaifa tukamwambia maridhiano, anakimbia maridhiano, hii sio sawa.” alisema Makonda.
Alihoji kwanini Mbowe anakubali fedha za michango ya Rais Samia Suluhu Hassan lakini hataki kuridhiana katika mambo ya Umoja wa kitaifa yanayoleta amani.
“Wanasema shukrani ya punda ni mateke, Mbowe alivyotoka gerezani siku ya kwanza moja kwa moja nimemuona yupo Ikulu, aliondokaje mule ndani, hatujui!, alikua na begi, hatujui!, gari alilotumia ni la nani, hatujui!, ila ninavyojua jinsi alivyo Rais Dk Samia Mbowe hakuweza kuondoka mikono tupu”
Alisema Mbowe huwa haondokagi mikono mitupu pale anapoenda Ikulu kuonana na Rais Samia Makonda.
Poa Makonda aliongeza kuwa kuwa haoni haja ya maandamano ya Chadema kwani sawa na kuivua nguo nchi.
“Mbowe kwanini unataka kuitia nchi yetu aibu, unataka kuandamana ili upate picha, uzipeleke Umoja wa Mataifa, kupeleka mambo ya nchi yetu huko,” alihoji Makonda
Makonda alieleza kuwa, hata kule ulaya anakotaka kwenda kupeleka mambo ya nchi yetu wamsaidie fedha, nako wanashida zao ikiwemo mgogoro wa vita, hivyo akubali kurudi katika maridhiano kudumisha na umoja wa kitaifa.
Alisisitiza kuwa sio vyema kuchezea amani tuliyonayo kwani yako mataifa yanatamani kuona nchi hii inakosa inavurugika wanatamani kuona ina migogoro wachukue mali wapelekee watoto wao.
Alibainisha kuwa, Tundu Lissu analalamika kwanini Mbowe na Mnyika wanahama agenda ya Uchaguzi kuingia katika maandamano ikiwa ni njama yake yakuendelea kubaki katika uwenyekiti wa Chadema.
Alieleza kuwa mafanikio na maendeleo ya Chadema yanatokana na matunda ya Rais Samia kuwawezesha kifedha kwa kuwalipa malimbikio ya ruzuku pamoja na kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi kuu ya Chadema.
Aliongeza “Tangu kuanzishwa kwa historia ya Taifa hili, miaka yote, hawajawahi kuwa na ofisi, miaka yote walikuwa wanaishi kwa kupanga, mwaka huu ndipo wameweza kununua ofisi yao ni matokeo ya Rais Dk.Samia kujenga maridhiano na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Sambamba na hayo pia Makonda aliwasihi wakazi wa Kilimanjaro kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwasababu amekuwa akiwapatanisha Watanzania bila kujali chama, kabila wala kipato na kila aliyemwendea na kulalamika alimsikiliza na kuchukua hatua.
“Nikisema upatanishi si jambo jepesi, si kwamba ndugu zetu hawakuitendea mambo mabaya CCM la hasha, wako vijana wa Chama chetu waliumizwa, walipigwa, wengine waliharibiwa hata mali zao, Dk Samia akasema hapana, sisi upande wangu kama mwenyekiti wa chama tunasamehe,”
“Mshangao wangu ni kuona ndugu zetu wapinzani kujiona wana haki ya kila kitu. Wana haki ya mawazo, mawazo yao ndio ya nchi, wana haki ya sheria, sheria wanayoitaka wao ndio ziwe za nchi, wenzao wakitaka hawana haki. Na demokrasia yao tafsiri yao ni kile ambacho wao wanakitaka, nje ya kile ambacho wao wanakitaka hiyo kwao sio demokrasia, wakati tafsiri ya demokrasia wengi wape, wachache wasikilizwe,” alisema Makonda.
Hivyo Makonda aliwataka wana Kilimanjaro wamuache Mbowe aendelee kufanya harambee za kanisani kwasababu ili harambee za kanisani ziwe na maana kwake lazima afike kwa watu wa CCM.
“Aliahidi kutoa pesa kanisani kama hajatoa mimi nitamsaidia kutoa kwakuwa Mbowe ni kakaangu,”
“Kaka yangu yule muacheni afanye harambee za kanisani na ili harambee za kanisani ziwe na maana kwake lazima aje CCM ,Naomba niulize swali mimi sikuepo kwani yeye alitoa shilingi ngapi ?, Basi kama aliahidi na hajalipa nitamsaidia kutoa kwa niaba yake yule ni kaka angu,Kaka angu Mbowe kwenye ela namjua na yeye anajua kuwa namjua,”alisema.
Aidha Makonda alimpokea, mjane wa Augustino Mrema, Doreen Agustino Mrema aliyeamua kujiunga na CCM akiambatana na wanachama wengine waliotoka vyama vya upinzani.
Mbali na hayo, CCM iliwalekeza wakuu wa mikoa wote kuwaelekeza wakuu wa wilaya watoke ofisini kwenda kukaa na wananchi kwenye maeneo yao kutatua kero zao kwasababu chama hicho kimebaini kwamba wanaofika ofisini kupeleka kero zao wanapangwa kwenye foleni na kusikilizwa kwaupendeleo kwakuwa wengine hawana kipato.