CCM yaonya longolongo Tanroads, Tarura

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita kimetoa angalizo kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha inatekeleza na kukamilisha miradi yake kwa wakati ili kumaliza kero ya barabara kama ilivyopangwa.

Aidha CCM imewataka Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) mkoani humo kuzingatia mikataba ya utekelezaji wa miradi ya barabara ili viongozi wa Chama hicho  watoe taarifa sahihi kwa wananchi wao.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicolous Kasendamila  ametoa maagizo hayo katika kikao cha wajumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita kilichofanyika mjini Geita.

Amesema ipo miradi ya barabara kwenye baadhi ya maeneo imechukua muda mrefu kukamilika tofauti na matarajio ya awali hali inayowafanya wananchi kuteseka kwa kutumia barabara za michepuko zisizo na ubora akitolea mfano ujenzi wa kilomita moja ya lami katika mji wa Kharumwa wilayani Nyang’hwale ambao haujakamilika tangu ulipoanza mwezi Juni 2023 ingali taarifa zinaonyesha serikali ilishatoa pesa za mradi.

Amesema,  zipo barabara zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha lakini ukarabati wake kwa Tarura na Tanroads umekuwa ni wa kusuasua na hivyo wananchi kusafiri kwenye mazingira magumu.

Kasendamila ameelekeza Tarura kutoa kipaumbele kwa barabara za kijamii zinazohudumia maeneo ya muhimu ili kuondoa kero kwa wananachi kushindwa kuzifikia huduma za kijamii zilizojengwa na serikali.

“Barabara inapochukua muda mrefu bila kukamilika inachukua taswira mbaya, barabara inapochelewa kukamilika inasababisha usumbufu kwa sababu inapojengwa kunakuwa na njia ya muda pekee.

“Barabara ya muda inakuwa siyo imara, labda kanakuwa kafinyu, watu wanasubiri kwa muda mrefu wanasubiri barabara yao, wametangaziwa barabara inajengwa kwa kiwango cha changarawe au lami lakini haikamiliki.”

Meneja wa Tarura Mkoa wa Geita, Mhandisi Chacha Moseti, amekiri kupokea maelekezo ya chama na kueleza bajeti ya mkoa imepanda kutoka Sh bilioni tisa mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh bilioni 18 mwaka 2021/22.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema tayari ameshakutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na kumueleza kero ya barabara kuharibiwa mkoani hapa na ameahidi kushughulikia.

Habari Zifananazo

Back to top button