CCM yaonya wanaojipitisha ubunge, udiwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya wanachama wa chama hicho wanaoanza kujipitisha kwa wananchi ili kutaka nafasi za ubunge na udiwani.

CCM imeagiza wananchi hao waache mara moja kwa kuwa muda wa kufanya hivyo bado hivyo wanakiuka taratibu na miongozo ya chama.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisema hayo Bukombe jana wakati wa ufunguzi wa ukumbi wa mikutano wa CCM wilaya hiyo na kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya kupumzikia wageni.

Mradi huo umefikia asilimia 80 ya ujenzi na hadi sasa umegharimu zaidi ya Sh milioni 200.

“Mnakiuka taratibu na kwa kweli tunawaona na tutawachukulia hatua za kinidhamu.

“Chama hiki kina taratibu zake muda wa siasa bado sasa hivi waacheni waliopo wafanye kazi ikifika 2025 nafasi zitatangazwa hapo itakuwa ni ruksa kwa kila mwanachama kugombea ila kwa sasa acheni fitna na uchonganishi,” alisema Chongolo.

Aidha, aliagiza watendaji wa halmashauri nchi nzima wasimamie fedha za miradi ya maendeleo zilizopelekwa kwenye halmashauri zao, kwani serikali ya CCM imetoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha nchi inakua na maendeleo kwa wananchi yanaonekana.

“Serikali inadhamiria kuifungua nchi kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana sasa hatutakuwa na muhari wala haya kwa wale watakaochezea fedha hizo.

“Sisi kama Chama kinachotawala, tunataka kuona wananchi wanapata huduma safi kwa wakati, hivyo hatutakuwa na mchezo na yeyote atakayechezea fedha hizo,” alisema Chongolo.

Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko alisema Jimbo la Bukombe limetekeleza miradi ikiwemo ya afya, elimu na miundombinu kwa zaidi ya asilimia 80.

“Sisi kwetu kaulimbiu yetu ni kusema na kutenda na kupitia msemo huu tumeweza kushirikiana na kuhakikisha tunakamilisha miradi ya afya, miundombinu na elimu shule za msingi na kata tumeziboresha,” alisema Biteko.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Saidi Nkumba alisema mradi huo ulianza Julai 2019 sambamba na ujenzi wa ukumbi wa mikutano mradi huo ulihusisha ununuzi wa samani za ndani ya ofisi na ukumbi.

Alisema mradi huo ulihusisha pia ujenzi wa nyumba ya kupumzikia wageni, ujenzi wa jengo la migahawa, bustani kuzunguka eneo la ofisi, ukarabati wa vyoo matundu 6, ujenzi wa uzio pia ujenzi wa mtandao wa maji na tangi lenye ujazo wa lita 10,000.

Habari Zifananazo

Back to top button