CCM yapokea kilio bei ndogo ya alizeti
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitafi kisha katika mamlaka husika ombi la wananchi mkoani Singida kwamba serikali itoze kodi mafuta ya kupikia yanayotolewa kutoka nje ya nchi.
Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisema hayo Mkalama jana baada ya Mkuu wa mkoa huo, Peter Serukamba kusema serikali ilihamasisha wakulima walime alizeti na ikawakopesha wakulima mbegu bora na sasa wanajiandaa kuvuna, lakini bei imeshuka.
“Tunaelekea kuvuna hainunuliki kwa sababu mafuta ya kupikia yanayoingia nchini hayatozwi kodi, tunaomba Wizara ya Fedha iyaweke kodi,” alisema Serukamba.
Chongolo alisema: “Hili la kodi ya mafuta ya kupikia nimelisikia nalibeba, tunaenda kuulizana na wahusika, tumehimizana vya kutosha na wakulima wameitikia kwa kulima alizeti nyingi, hatuwezi kuwaangusha.”
Serukamba alisema msimu huu wa kilimo wamelima ekari 631,000 za alizeti kwa wilaya za Iramba na Mkalama, lakini umaskini kwa wananchi hautaondoka iwapo bei ya alizeti itaendelea kuwa chini kama sasa. Mkulima wilayani Mkalama, Magreth Msengi alidai bei ya gunia la debe saba alizeti kwa sasa ni Sh 55,000 hadi 60,000.
Alidai kuwa awali kabla ya mafuta ya kupikia kutoka nje kuruhusiwa kuingia nchini bila kodi, alizeti hiyo iliuzwa kati ya Sh 65,000 hadi 80,000. Akizungumza katika mkutano wa Shina Namba Tano wilayani Mkalama, Chongolo alisema mwaka 2015 walizunguka nchi nzima kunadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayotekelezwa sasa na kazi ya chama ni kuzunguka kukagua utekelezaji wake.
“Sisi sio chama cha maneno, tunatekeleza ilani tuliyoinadi na sasa serikali inaitekeleza, tunakagua kuona changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi hii ndio kazi yetu,” alisema Chongolo.
Akizungumzia changamoto ya Barabara ya Nduguto-Iguguno, alisema itajengwa hadi Sibiti mpakani mwa Singida na Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.