KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema Chama hicho kinaridhishwa na kasi ya ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendo kasi(SGR) ambayo ujenzi wake unakwenda vizuri na watu waliokuwa wanabeza ujenzi huo wamepata aibu ya mwaka.
Shaka amesema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kilosa alipokuwa akizindua msimu wa kilimo mkoani Morogoro.
Amesema pamoja na kuzindua msimu wa kilimo, amepata nafasi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama hicho ya mwaka 2020/2025 na kasi ya ujenzi wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ukiwemo wa reli ya kisasa na ujenzi wa barabara ya lami ya Dumila-Kilosa.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya kazi kubwa na nzuri kuhakikisha anaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati na kasi inakwenda vizuri,”amesema Shaka.
“Kubwa kuliko yote aibu ya mwaka, kuna watu waliaminisha watu kwamba miardi ya mikakati haitakwenda itakwama.Nimekagua ujenzi wa reli ya mwendo kasi , mambo yanakwenda vizuri sana , na juzi tumesikia majaribio yaliyofanywa na Kamati ya Bunge kutoka Dodoma mpaka Dar es salaam.
“Mambo yameiva wananchi wa maeneo mbalimbali ambapo reli hii inapita wakiwemo wananchi wa Kilosa jiandaeni kutumia fursa kutokana na kukamilika kwa miundombinu ya barabara, kukamilika kwa reli ya mwendo kasi, kwa fursa hizi naamini hata umasikini utakuwa ni wa mtu kujitakia mwenyewe,amesema Shaka.
Ameongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ni wazi Rais Samia ameonesha njia,amewafungulia dunia na kubwa zaidi anawatoa wananchi kwenye wimbi la umasikini.
Shaka amesisitiza reli ya mwendo kasi ikianza na miundombinu ya barabara imekamilika wananchi wa Kilosa na maeneo mengine watafanyabiashara , watasafirisha mazao na bidhaa nyingine kwa haraka , pia watafanya uwekezaji.
“Hivyo fedha itapatikana na mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa.“Lazima mjiandae kisaikolojia kupokea hizo fursa ambazo Rais Samia amewapatia.”
Aidha Shaka amesisitiza yote ambayo Rais Samia amekuwa akiyafanya katika kutekekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 2020-2025.
“Yote ambayo Chama chetu kiliweke msisitizo kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu Rais Samia ameendelea kutekeleza kwa vitendo, nataka niwaambie katika eneo ambalo Chama chetu siku zote hakifanyi makosa ni eneo la kuwapata viongozi ndani ya nchi hii na mustakabali wa kuongoza nchi yetu umejengwa na CCM.”