CCM yasifu kazi daraja la Kigongo- Busisi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Magufuli lililopo maeneo ya Kigongo Busisi mkoani Mwanza.

Daraja hilo linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita ujenzi wake umefikia asilimia 51 na linatarajiwa kukamilika Februari mwaka 2024.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana alisema chama hicho kinaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa daraja hilo na ana imani utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Kinana alisema litakapokamilika mwaka 2024 nchi itakuwa imepata alama ya kuwa na daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki likiwa na urefu wa kilomita 3.2.

“Najaribu kukumbuka madaraja mangapi katika Afrika yenye urefu huo kama hili halitakuwa la kwanza basi litakuwa katika tatu bora. Hivyo niwapongeze wote wanaoshiriki ujenzi wa daraja hili ndugu zetu wa kutoka Korea, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajenzi kutoka Kampuni ya China na Watanzania wote wanaoshiriki,” alisema.

Aliongeza: “Mnafanya kazi nzuri sana, mnafanya kazi kubwa na Rais (Samia Suluhu Hassan) amenituma nije niwasalimie na niwaambie kwamba anangojea aje kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa daraja hili litakapokamilika, daraja hili litakapokamilika litaziunganisha wilaya mbili za Sengerema na Misungwi ambazo zinatenganishwa na Ziwa Victoria kwa kupitia barabara ya Usagara, Sengerema hadi Geita,” alisema Kinana.

Awali Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa daraja hilo, Abulkarika Majuto alisema ujenzi huo kwa sasa umefikia asilimia 51.

Majuto alisema daraja la JP Magufuli lina urefu wa kilomita 3.2 na barabara unganishi za kilomita 1.66.

Alisema barabara ya Usagara, Sengerema hadi Geita ni miongon

i mwa barabara ambazo zinapita katika ukanda wa Ziwa Victoria na utekelezaji wake ni miaka minne ambapo unatarajia kukamilika Februari 24, mwaka 2024.

Ujenzi wa miradi ya madaraja ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).

Ilani hiyo katika ukurasa wake wa 67 na 68 inabainisha miradi ya madaraja iliyokamilika kujengwa na ile inayoendelea kujengwa wakati Mpango wa Maendeleo (Uk 31) ukieleza kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa madaraja makubwa 12.

Mpango huo wa Maendeleo pia unatambua kuendelea kwa shughuli za ujenzi wa madaraja kadhaa likiwemo la Kigongo–Busisi, Sukuma, Simiyu, Mkenda, Mtera, Godegode, Malagarasi Chini na Ugalla.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button