CCM yataka bodaboda, bajaji zitumie gesi

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuona namna ya kuweka mfumo wa gesi asilia kwenye pikipiki na bajaji ili kuwasaidia wananchi wengi wanaotumia usafiri huo.

Pia amezitaka kampuni nchini kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujazia gesi hiyo ili kupunguza gharama za uagizaji wa mafuta ili kuwapunguzia usumbufu watu wanaotumia mfumo huo.

Akizungumza katika ziara Jumatatu Dar es Salaam, Shaka alisema uwekaji wa mfumo wa gesi kwenye pikipiki na bajaji utawasaidia madereva kubana matumizi kwani kupanda kwa mafuta kunasababisha kupanda kwa gharama za maisha.

Shaka alisema teknolojia hiyo itasaidia kupunguza gharama na kwamba itawatoa kiuchumi kama taifa kutokana na vita ya kiuchumi inayoendelea duniani.

Alisema Tanzania ina akiba ya futi trilioni 57.5 ya gesi asilia hivyo imeifanya Tanzania kuwa nchi ya 82 duniani inayotumia gesi asilia katika magari na uzalishaji wa umeme.

Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba alisema wameanzisha vituo viwili vya umahiri katika Tehama Afrika Mashariki kwa kubiasharisha bunifu na mazao ya ngozi ili waweze kujitegemea kiuchumi.

Alisema mradi wa gesi asilia ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali katika jamii na kwamba serikali imewekeza fedha kwa ajili ya kuanzisha vituo hivyo.

“Hii ni kampuni ya kimkakati kwani unasaidia kupunguza utegemezi wa mafuta ya dizeli na petroli kutokana na vita vya kiuchumi vinavyoendelea. Mpaka sasa zaidi ya magari 1,000 yamewekewa mfumo wa gesi asilia kwani tuna gesi ya kutosha ambayo itatusaidia kuepuka utegemezi,” alisema Profesa Ndomba.

Meneja Mradi wa gesi asilia (CNG), Dk Esebi Nyari alisema mfumo huo umelenga kuondoa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na mafuta na kwamba gesi inasaidia kupunguza gharama na ni salama kwa matumizi.

Dk Nyari alisema wako katika mkakati wa kubadili mfumo wa dizeli kwenda kwenye gesi na kwamba wanaendelea na tafiti ya kuweka mfumo huo katika bajaji, bodaboda na treni.

“Gharama ya gesi kwa kilo moja ni Sh 1,550 na tuna mpango wa kupunguza gharama hiyo iwe Sh 1,230 ili watu wengi waweze kuhamasika kutumia mifumo ya gesi asilia. Tunaiomba serikali kuendelea kuhamasisha wawekezaji kujenga vituo vya usambazaji wa gesi hiyo,” alieleza Dk Nyari.

Alisema kampuni 15 zina vibali vya kujenga vituo nchini ikiwemo kuongeza vituo vitano vya kujaza gesi Dar es Salaam kutoka vilivyopo sasa vya Ubungo na Tazara.

 

Habari Zifananazo

Back to top button