CCM yataka Msajili achunguze fedha Chadema

DAR ES SALAAM; CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ashirikiane na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kuchunguza fedha chafu zinazodaiwa kuingizwa kwenye uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na CCM.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema hayo jana alipozungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kilichorushwa na kituo cha UTV cha kampuni ya Azam Media Dar es Salaam.

Makalla alikuwa akijibu tuhuma zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu kuwa CCM inahusika kuingiza fedha chafu wakati chama kikielekea katika uchaguzi mkuu wa chama.

Aliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama na Takukuru wawe pamoja na mtoa tuhuma ambaye ni Lissu ili wasaidiane kuufahamu ukweli kuhusu fedha hizo kuwa ni shilingi ngapi, zimewekwa na nani kwa sababu ni hatari kwa chama kupokea fedha chafu.

“Kama chama kinaweza kupokea hela chafu maana yake ni kuwa hakiwezi kuwa na dhamira nzuri kwa wananchi. Kwa mantiki hiyo sidhani kuwa Chadema itatoka salama kwa sababu wanatuhumiana wenyewe,” alisema Makalla.

Alisema kutokana na tuhuma hizo Chadema imetuma ujumbe kwa wananchi kwamba chama hakipo salama kutokana na mgawanyiko uliopo ndani ya chama.

Makalla alisema kwa kuwa tuhuma zimetolewa na mtu mkubwa ndani ya chama ambaye ni Makamu Mwenyekiti, hakuna haja ya CCM kujibu tuhuma hizo kwa kuwa Chadema ndio inaingiziwa fedha hizo.

Makalla alisema pamoja na kwamba Chadema wamejituhumu wenyewe wameingiziwa fedha chafu, wanatakiwa watoe ushahidi wenyewe ili sheria zichukue mkondo wake.

Alimtaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ajitokeze ama kukanusha au kukubali tuhuma kuwa chama kimepokea fedha chafu. Makalla alisema ikiwa Mbowe atakubali kuwa chama kimepokea fedha chafu, aseme zilikotoka, kiasi na dhumuni la fedha hizo.

Habari Zifananazo

Back to top button