CCM yataka viwanda vya pamba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesudia kuzungumza na Serikali Kuu kuona namna ya kujenga viwanda vya ndani vya kuchakata zao la pamba ili kunusuru uhai wa bei ya zao hilo.

CCM imefikia hatua hiyo kufuatia malalamiko ya wakulima wa zao hilo wilayani Itilima mkoani Simiyu kuhoji juu ya zao hilo kutokuwa na bei elekezi jambo linalosababisha kila msimu kuuza kwa bei ya chini na hata wakiuza malipo wanalipwa nusunusu.

Advertisement

Mkulima Ndula Masuke akizungumza katika mkutano huo amesema ameacha kulima zao hilo kwa kuwa limemfilisi hata wanawake wamemkimbia hana hela, na pia hata pembejeo za zao hilo ni changamoto.

Amesema dawa wanazopelekewa kwa ajili ya zao la pamba zipo chini ya kiwango kwani wanapulizia ndani ya muda mfupi magonjwa kama funza wanaendelea kushambulia.

Hoja iliyoungwa mkono mkulima, Sagata  John na kudai kama bei elekezi inasimamiwa na serikali au chama inakuwaje elimu inashindwa kutolewa muelekeo wa bei na kuacha wakulima wakiendelea kutaabika?

“Serikali imekuwa kimya na chama chake hawataki kuja kutoa elimu bei imeshuka na tunapaswa kufanya Nini? Wametusaliti tukipambana na madalali kila kukicha na hakuna wakutusaidia.” alihoji

Sagata amesema licha ya kuwa mkulima wa pamba lakini anajihusisha na uchimbaji wa madini na wanapokuwa kwenye shughuli hizo kuna kuwa na bei elekezi na wanapokwenda kuuza wanaangalia kwenye mtandao soko la dunia linasemaje?

“Kwanini bei ya pamba haijawekwa kwenye mfumo wa kidigitali Ili mkulima anapoenda kuuza awe anajua kilo moja  inauzwa kiasi fulani kuwarahisishia wakulima wanapoenda kuuza wawe wanajua ili wasiendelee kujibiwa,

Akijibu maswali hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Laini Wilaya ya Itilima, Makamu Mwenyekiti wa (CCM)Tanzania Bara, Abdurlhaman Kinana amesema changamoto hiyo inapaswa kutatuliwa na Serikali Kuu na kwamba atalifikisha.

“Jambo hili si la kwenu wakulima isipokuwa ni la Serikali Kuu na mimi nalichukua kwenda kuonana na wakubwa kuwaambia wakulima wanalima bei inashuka kwa sababu hakuna viwanda nchini,”

“Serikali Kuu inapaswa kujitahidi kujenga viwanda vya kuchakata zao la pamba ikiwemo kutengeneza nyuzi na nguo ili wakulima wasitegemee  soko  la nje ya nchi  pekee  katika kuuza.

Amesema, kuendelea kupeleka pamba kwenye soko la nje ya nchi kuwauzia wakubwa ni wazi  bei ya zao hilo itaendelea kuwa ya chini kwa kuwa wao wanapanga wanunue malighafi hiyo kwa bei  chini.

“Jibu lingine la bei nzuri ya zao hili kila mkulima anatakiwa kulima kilimo cha kisasa mfano nimeona Singida kuna mkulima mmoja anapata kilo 1000 wakati Mkuu wa Mkoa wa Simiyu aliyelima baridia heka moja alipata kilo 500.

“Wewe unayelima hapa kwa utaratibu wako heka moja unapata kilo 150 hamuwezi kufanana kimapato, sasa ni kazi ya serikali kuwaleta wataalamu wawafundishe wananchi walime kilimo cha kisasa,” amesema.

Amesema  kutoka na changamoto hiyo anakusudia kuonana na Waziri wa Kilimo kuongea naye kuhusu kusuasua kwa malipo ya zao hilo kila baada ya kuuza zao hilo.

Amesema kendelea kulipwa nusunusu kila wanapouza pamba ni kwamba zao hilo linakosa thamani na kuendelea kuwasumbua wakulima wanaotumia gharama kubwa katika uendeshaji.

Mkurugenzi Mkuu  wa Bodi ya Pamba, Marko Mtunga amesema asilimia 80 ya zao hilo inayozalishwa nchini inapelekwa nje ya nchi ndiyo maana hakuna bei elekezi inayojulikana.

Amesema mwaka huu wa fedha serikali imeanzishwa mfuko wa kilimo wa kunusuru bei za mazao japo itachukua muda kuwa na uwezo lakini moja ya kazi yake ni kudhibiti soko na kuwafanya wakulima kuwa na uhakika.

“Mfano bei ya soko ni 1,200 lakini ikaporomoka na kuwa sh 1,000 mfuko unajazia sh 200 ili kunusuru wakulima kuuza bei ya hasara.” Amesema

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *