CCM yateua wagombea jumuiya zake

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) imeteua majina ya wanachama wake watakaogombea nafasi za uongozi katika jumuiya za chama hicho ngazi ya taifa.

Taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka jana ilieleza kuwa CCM ilifanya uteuzi huo katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Taarifa ya Shaka kwa umma ilieleza kuwa katika kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya CCM, Dodoma, kwa mujibu wa katiba ya CCM ya mwaka 1977, toleo la mwaka 2022 Ibara ya 82(1) wanachama wanne wameteuliwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM taifa.

Shaka aliwataja wanachama hao kuwa ni Farid Haji, Kassim Kassu, Mohamed Mohamed na Abdallah Natepe.

pharmacy

Walioteuliwa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti UVCCM Taifa ni Khadija Ismail, Dorice Mgetta, Victoria Mwanziva na Rehema Omary.

Shaka alitaja walioteuliwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) taifa ni Gaudentia Kabaka, Kate Kamba, Dk Wemael Chamshama, Mariam Lulida na Mary Chatanda.

Walioteuliwa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UWT taifa ni Latifa Ahmed, Thuwaybah Kissasi, Hafsa Khamis na Zainab Shomari.

Shaka alitaja walioteuliwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti Wazazi Taifa ni Dk Edmund Mndolwa, Fadhili Maganya, Bakari Kalembo, Said Mohamed Mohamed, Mwanamanga Mwaduga, Ally Othman, Ali Masudi, Hassan Zahara.

Walioteuliwa kugombea nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti Wazazi taifa ni Haidar Abdalla, Dk Wemael Chamshana, Fatma Haji, Rachel Kabunda, Neema George Mturo, Zahoro Mohamed na Dogo Mabrouk.

“Uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hizo kwa ngazi ya Taifa utafanyika tarehe 24-29 Novemba, 2022,” alieleza Shaka.

Taarifa hiyo iliwakumbusha wagombea wote waheshimu kanuni za uchaguzi za CCM na misingi ya chama kwa kufanya siasa safi na kuzingatia maadili ya chama wakati wote.

“Aidha orodha ya majina ya wagombea uongozi wa chama na jumuiya zake ngazi ya mkoa yatatumwa katika mikoa husika,” alisema Shaka.

Habari Zifananazo

Back to top button