CCM yatoa mwelekeo wa vijana 2030

DAR ES SALAAM: MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Rehema Sombi, amesema CCM imeendelea kuisimamia serikali kuchukua hatua za kujenga ustawi na maendeleo ya jamii kwa kuimarisha huduma kwa makundi maalumu likiwemo la watu wenye ulemavu, vijana, watoto, wanawake na wazee.

Rehema ameyasema hayo leo Septemba 25, 2023 katika kikao kilichoambatana na hafla ya kampeni ya uwekaji wa bendera ya malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals – SDGs) iliyofanyika katika jengo la Umoja House – Ubalozi wa Netherlands.


Amesema baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni kuendelea kutoa ruzuku kwa taasisi za watu wenye ulemavu kila mwaka na kutoa vitendea kazi, pamoja na kuanzisha mfuko maalumu wa watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi ikiwa ni sera za mwelekezo wa CCM 2020 -2030.

Advertisement

“Hatua nyingine ni kutekeleza Sera ya jinsia ya mwaka 2016 ambayo inatoa mwongozo wa kusimamia masuala yote ya wanawake nchini, kuanzisha mtandao wa wajasiriamali wanawake na kutekeleza mpango kazi wa miaka mitano wa kupambana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto (2017 – 2022),” amesema.

Pia, ametaja hatua nyingine ni kutoa mafunzo ya stadi za maisha kwa vijana 79,675 na kuviwezesha vikundi vya vijana 796 vinavyojishughulisha na kilimo, ufugaji na ushoni kupata mikopo kupitia mfuko wa uwezeshaji hivyo kufanikiwa kujiajiri katika maeneo ya kilimo.


Pamoja na hayo ameonyesha msimamo wa serikali katika kuweka mkazo juu ya masuala ya elimu hususani ya sayansi kwa wasichana.

Aidha, amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka juhudi kubwa kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu hususan kupitia ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kimaendeleo na kushirikisha vijana katika ukuzaji uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mkutano huo umeongozwa na Balozi wa Netherlands nchini Tanzania Wiebe De Boer ambaye amesisitiza kuwa vijana ndilo kundi muhimu kwa mabadiliko ya maendeleo kwa nchi yao.

3 comments

Comments are closed.