CCM yatoa tamko maeneo ya wawekezaji yasiyotumika

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza serikali kuchukua maeneo yote ambayo wamepewa wawekezaji na hawayatumii.

Agizo hilo limetolewa leo Julai 25,2023 na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Dareda wilayani Babati, mkoani Manyara.

Kinana amesema: Kuna  maeneo yamekaa bure na watu  wanaojiita wawekezaji hawayatumii na inawezekana wanayakodisha, hawana haki ya kukaa nayo.

” Nitampigia simu Waziri wa Ardhi ( Angelina Mabula), ashughulikie suala hili, wote ambao hawatumii maeneo yaliyopewa wanyang’anywe.” Ameongeza.

“Mimi najua mwekezaji wa kwanza ni mtu anayewekeza nguvu na jasho lake ambaye ni mkulima, lakini baadhi ya wawekezaji wamepewa ardhi kuzalisha, badala yake wanakodisha huu ni nyonyaji. “

Akifafanua amesema anachukua hatua hiyo kwa vile Chama ndicho kinachoiangiza serikali na serikali haina mamlaka ya kukiagiza Chama

Kauli ya Kinana imekuja baada ya Mbunge wa Babati Daniel Sillo kuwasilisha taarifa ya Jimbo lake na  kuelezea changamoto zilizopo ikiwemo migogoro ya hardhi katika hifadhi ya Tarangire.

Aidha, Kinana amemuagiza Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa kushughulikia haraka mgogoro huo.

Habari Zifananazo

Back to top button