CCM yavunja ukimya sakata la Gekul

DAR ES SALAAM: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitosita kuchukua hatua dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Babati mjini, Pauline Gekul iwapo tuhuma zinazomkabili zikiwa ni za kweli.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akizungumzia kuanza kwa vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya Chama hicho kuanzia leo na kesho.
Kuhusu mbunge wa Babati amesema Chama kina taratibu na kanuni hivyo likifika ngazi ya taifa watalitolea taarifa.
“Kwa tuhuma za mbunge huyo ni kwamba Chama kina taratibu na kanuni na sisi ngazi ya taifa tunajua kuna mashina zinazoanza ngazi tawi, Wilaya, Mkoa na ikifika hatua ya taifa tutaweza kutoa taarifa,”amesema.
Ameongeza kuwa kanuni zipo na wanayo timu na mamlaka za nidhamu na watu wa maadili , kama kuna jambo litabadilika taratibu zitafua mkondo wake.
Jumamosi ya wiki iliyopita,Rais Dk.Samia alitengua nafasi ya Unaibu Waziri wa Katiba na Sheria iliyokuwa ikiongozwa mbunge huyo.
Kuhusu vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM amesema Chama kimekaribisha wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu katika mkutano wake wa kawaida chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Amesema kikao kitaanza na semina ya mafunzo ya wajumbe wa Halmashauri Kuu leo na kesho kutwa kufuatiwa na kikao Cha Kamati Kuu kitakachoongozwa na Rais Dk.Samia, Dar es Salaam.
 
Pia vikao hivyo vimetanguliwa na sekretarieti ambacho kilikaa jana chini ya Katibu Mkuu wa Chama, Daniel Chongolo.
 
Makonda amesema maandalizi yote yamekamilika na kikao hicho kitajadili mstakabali wa uhai wa Chama na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Back to top button