CEO mpya Simba aahidi raha

Simba watakiwa kutanguliza mbele maslahi ya klabu

OFISA Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa klabu ya Simba, Imani Kajula ametangaza mikakati yake na kusisitiza kazi yake itakuwa kuiunganisha Simba na wafanyabiashara pamoja na kampuni mbalimbali kuwekeza.

Kajula ameyasema hayo kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama wa klabu hiyo leo kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyeyere, Dar es Salaam  hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu atangazwe kuchukua wadhifa huo, akichukua nafasi ya Barbara Gonzalez.

“Tunataka tushinde, lazima kujenga timu bora, lakini kazi ya pili ni kujenga taasisi imara na endelevu hata nisipokuwepo kuwe na mtu mwingine wa kuendeleza, lakini pia kujenga chapa imara na kuongezea mapato na kingine ni kuongeza wadhamini wengine ambayo ni moja ya majukumu yangu.

Advertisement

“Pia lengo ni kuifanya klabu kuwa na fedha zakutosha, ili kufanya mambo yetu kwa urahisi,” amesema Kajula.

Mtendaji huyo pia ameeleza kuwa mikakati yake mingine ni kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kama ilivyofanya timu yao ya wanawake ‘Simba Queens’ mwaka jana, hivyo ni lazima waekeze nguvu katika kuandaa programu maalumu zitakazowasaidia kufikia malengo hayo.

Kajula amesema lengo lao msimu huu ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu na kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wanataka kufika robo fainali au zaidi ya hapo, wakati kwa  Simba Queen wanataka  kufanya vizuri zaidi Afrika na kuboresha timu za vijana.