Chadema yasifu misingi yao

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe amesema yeye na viongozi wenzake hawawezi kumvutia mtu kujiunga na chama hicho bali misingi ya chama ndiyo nguzo kuu ya kumfanya mtu aweze kujiunga.

Mbowe ameyasema hayo katika mwendelezo wa ziara ya chama hicho nchi nzima wakati wa ziara yake mkoani Katavi alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Manispaa ya Mpanda katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kashato.

Amesema misingi hiyo ni haki, uhuru, utawala wa demokrasia na maendeleo huku akisema kila Raia wa Tanzania anao uhuru wa kuamua maisha yake, uhuru wa kutoa mawazo bila kuingiliwa na mtu yoyote.

Aidha, Mbowe amesema CHADEMA ni chama cha haki hivyo kila anayeguswa nacho lazima awe mtu wa haki na kuhakikisha inatendeka kila eneo ikiwemo kwa wafanyakazi, watoto, wakulima, mahakamani, Polisi na kwenye ajira.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu, amesema suluhu ya matatizo na changamoto zote zinazotokea nchini ni katiba mpya.

Chama hicho kikiwa na msafara wa viongozi mbalimbali wakioongozwa na Mwenyekiti wake Taifa Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, Katibu wa Chama Zanzibar Salumu Mwalimu na Katibu Bara John Mnyika watakuwa na ziara ya siku nne mkoani humo huku ajenda kuu ikiwa ni Oparesheni +255.

Habari Zifananazo

Back to top button