Chadema yawatolea macho wana CCM wawili Iringa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataja wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wawili kinaowamezea mate, mjini Iringa.

Wanachama hao ni pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas na mfanyabiashara Ahamed Huwel.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu aliwaomba wana CCM hao wajiunge na chama chama ili kwa pamoja waharakishe maendeleo ya wana Iringa na Taifa kwa ujumla.

Katika mkutano wao wa hadhara uliofanyika jana mjini Iringa na kuhutubiwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, Sugu alisema wana CCM hao wanaweza kuguswa na kushughulikia matatizo ya wana Iringa kwa nafasi zaidi wakiwa Chadema na akawaomba wajiunge na chama chao pamoja na kutambua ugumu wa jambo hilo.

Mbali na siasa umaarufu wa Asas mkoani Iringa umesambaa kila kona kwa namna anavyochangia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali za maendeleo na kutoa misaada yake kwa mtu mmoja mmoja na makundi mbalimbali ya kijamii.

Na Huwel anafahamika kwa jinsi alivyoshughulikia tatizo la maji katika tarafa za Idodi na Pawaga pamoja na mkakati wake wa kuendeleza kilimo cha Tumbaku wilayani humo.

Wakati huo hu Mbowe amezungumzia sera yao ya majimbo huku akiibua tena mjadala wa lugha ya kufundishia nchini.

Katika hotuba yake kwa wana Iringa Mbowe alisema hakuna namna Tanzania inaweza kujitenga na matumizi ya lugha ya kingereza kama lugha ya mawasiliano na biashara duniani.

“Hata katika nchi za amerika na ulaya zilizoanza kufundisha kiswahili, walimu wanaotakiwa huko ni wale ambao mbali na kujua kiswahili lakini ni lazima wajue ipasavyo kingereza,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button