“SAMAHANI Waiter ongeza glass
Eh muhudumu ongeza glass
Mmhh Samahani Waiter ongeza glass
Eh muhudumu ongeza glass.
“Acha nilewe nilewe tuu
Eh nilewe nilewe tu
Acha nilewe nilewe tu
Nilewe nilewe tuu
Eh nilewe nilewe tu
Acha nilewe nilewe tu
Nilewe nilewe tuu.Nilewe nilewe tuu,” hiyo ni sehemu ya vibwagizo katika wimbo uitwao Muhudumu wa msanii Aslay Isihaka Nassoro a.k.a Dogo Aslay.
Sio kwamba nataka nikufundishe kuimba au nimekuwa mwimbaji hapana! Bali nataka nihusishe kibwagizo cha wimbo huo hasa kama umeiangalia ile video yake, ambapo inaonesha ugomvi kati ya Dogo Aslay na mpenzi wake, ambapo karibu beti zote Dogo Aslay analalamika kuhusu mpenzi wake, hadi baadaye anaenda kwenye kilabu cha pombe za kienyeji huko ndo anajiliwaza akitaka aongezwe glasi.
Hakika Dogo Aslay anapata ulabu wa kutosha, anajifariji kwa kilichomkumba na maisha yanaendelea kusonga. Sitaki beti za wimbo huo, nataka kibwagizo tu. Ongeza glasi!
Tuachane na hiyo hadithi ya kufikirika ya Dogo Aslay, ambayo pengine haina uhalisia, nataka nikupeleke katika tukio ambalo lina uhalisia, halifanani na la Dogo Aslay, lakini lenyewe ni kama linakolezwa na kile kibwagizo cha ‘Ongeza Glasi’, yaani maana yangu unasikia raha hadi unataka uongezwe glasi.
Ndiyo kinaongezwa glasi. Nini hicho kinachoongezwa glasi? Ni mila ya Chagulaga, ambayo jamii inayo, inaijua si nzuri, njia za kudhibiti zinajulikana lakini wapo baadhi ya wazazi wanaongeza glasi. Wanaikoleza, wanataka iendelee tena na tena licha ya kwamba inachefua hata kuisikia.
Chagulaga ni mila na tamaduni ya jamii ya Wasukuma, ambayo imeelezwa kuongeza mimba za utotoni na vifo vitokanavyo na uzazi mkoani Katavi na maeneo mengine Kanda ya Ziwa, huku wananchi wakiiongezea glasi!
Mila hizo msichana akivunja ungo basi huandaliwa sherehe za ngoma za kimila hasa kipindi cha mavuno, ambapo wasichana na wanaume hujipanga, mwanaume hunyoosha mkono, ambapo binti atamchagua mwanaume na kuanzisha naye mahusiano.
Hata hivyo kwa sasa utamaduni huo umekua mwiba mchungu kwa mabinti mkoani Katavi, ambapo akivunja ungo tu wazazi hutafuta vijana kadhaa na kumlazimisha binti kumchagua mmoja na asipofanya hivyo huadhibiwa kwa viboko na adhabu nyingine kali.
Akizungumza katika mahojiano maalum na HabariLEO , Ofisa Tabibu wa Zahanati ya Utende Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Neema Sanga, anasema binti asipofanyiwa chagulaga mama anaenda kwa mganga kwa kile wanachodai binti atakua na nuksi kwa nini mtoto hajachumbiwa.
“Ndio maana watoto wanapata mimba mapema, mtoto miaka 14 akivunja ungo tu anaozeshwa kwa lazima, atapangiwa wanaume 10 na kulazimishwa kumchagua mmoja, asipofanya hivyo anapewa adhabu kali,” amesema Neema na kuongeza:
“Mila na desturi hii ya chagulaga inahitaji nguvu za ziada, ukiwapa elimu wanakuona mtu wa kisasa, jamii inakutenga, ” amesema.
Kufuatia hali hiyo ya mimba za utotoni, Katavi ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vifo vya wajawazito na mimba za utotoni kwa asilimia 45 ikifuatiwa na Tabora asilimia 43 na Mara asilimia 37, kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (TDHS-MIS)
Kuna madhara makubwa yatakanayo na mimba za utotoni zikiwemo za kiuchumi, kisaikolojia, kiakili na kiafya.
Wataalamu wa afya ya uzazi wanashauri ili kuepukana na matatizo ya kiafya ni vyema kupata mimba baada ya kufikisha angalau umri wa miaka 18.
Chini ya miaka 18 msichana bado hajakomaa kiakili na kimwili kuweza kubeba majukumu ya malezi, pia nyonga huwa changa na nyembamba hivyo kutoweza kubeba kiumbe na kusababisha madhara makubwa wakati wa kujifungua.
Madhara mengine ya kiafya yatokanayo na mimba za utotoni ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, Fistula,kifafa cha mimba na vifo vya mama na mtoto.
INACHOSEMA JAMII
Kulwa Blanket (56) anasema mke wake wa kwanza alimpata kwenye chagulaga.
“Chagulaga ndio utamaduni wetu, hata mke wangu wa kwanza nilimpata kwenye chagulaga, huyu mwingine nilimuona nikampenda tu nikafuata taratibu za kawaida za kuoa, ” anasema na kuongeza:
” Ni ngumu kuacha mila hii, kukiwa na ngoma au harusi au sherehe za kimila ndio chagulaga hufanyika huko, utampa mkono binti ishara ya kumchumbia naye ataupokea hapo utawambia wanaume wenzako kuwa binti kanikubali hivyo wasimfuatile.
“Kama binti hatopokea mkono basi utaondoka na mwanaume mwingine ataenda kumpa mkono, ” anasema Blanket ambaye anaonekana kuifurahia mila hiyo
VIPI KUHUSU MABINTI
Lilian Charles (22) mkazi wa Uzega vijijini, anasema mila hiyo ni kandamizi na inawanyima mabinti fursa ya kusoma na kujiamulia mambo yake mwenyewe.
“Nina rafiki yangu tulipomaliza shule ya Msingi tu wazazi wake wakampelekea wanaume achague, alipelekewa wanne lakini hakua anampenda hata mmoja aliwakataa, walimfosi kwa kipigo mpaka akakubali, yaani ukipelekewa lazima uchague utake, usitake,” amesema na kuongeza:
” Natamani serikali ingeifuta mila hii isiwepo kabisa, binti miaka 14 unakuta ana watoto wawili au watatu, miaka 22 watato watano, wanalazimishwa kuolewa kwa sababu ya mali, ” anasema Lilian.
Asteria, mwenye miaka 19, alilazimishwa na baba yake kuolewa akiwa na miaka 16, akiwa anasoma kidato cha kwanza.
“Baba yangu hakuwa na pesa ya kunisomesha,” amesema. “Kisha nikagundua alikuwa amekwisha pokea mahari ya ng’ombe 20 kwa ajili yangu….: “Huku ni kawaida msichana akivunja ungo tu familia inalazimisha kuolewa ili wapate mahari.
“Kwa sababu hawathamini elimu ya mabinti zao, na kwa sababu pia zinaogopa wangepata mimba na kuleta aibu kwenye familia.
“ Wasichana wengine pia wanaona ndoa kama njia ya kutoka kwenye umaskini, ukatili, utekelezaji au utumikishwaji wa watoto,” anasema.
Sarah John ( sio jina halisi) , alilazimishwa kuolewa akiwa na miaka 15 baada ya kufeli mtihani wa kuhitimu darasa la saba
“Baba yangu aliamua kunitafutia mwanaume wa kunioa kwa sababu nilikuwa ninabaki nyumbani sifanyi chochote,” amesema.
Hata hivyo, idadi kubwa ya mabinti ambao wamefanya mahojiano na HabariLEO wamesema waume wao wamewatelekeza na kuwaacha wawatunze watoto bila msaada wowote wa kifedha.
Serikali inapaswa kufanya kazi ili kufanya maboresho ya sheria za ndoa na talaka, ikiwemo kuweka umri mdogo wa ndoa kuwa miaka 18
MRATIBU WA WILAYA ALONGA
Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Wilaya ya Mlele, Nuruel Sarwati anasema ng’ombe ndio chanzo cha mabinti kuolewa umri mdogo na hivyo kupitia changamoto mbalimbali wakati wa kujifungua zinazosababisha vifo vya watoto na wajawazito.
Amesema katika kipindi cha miezi nane kati ya Januari hadi Agosti jumla ya vifo vya watoto ni 49 na wajawazito wawili.
Amesema katika miezi hiyo watoto waliozaliwa na kufariki hapo hapo ni 14, watoto waliofia tumboni ni 21 na wale wa siku moja mpaka siku saba ni 14 na hivyo kufanya idadi ya watoto waliofariki kufikia 49, huku wajawazito waliopoteza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi ni wawili.
” Watoto wa huku hawasomi, wengi ni jamii ya kifugaji, tunapokea sana leba mabinti umri miaka 14, 15, 16 amezidi sana 17, ni changamoto, na hii ni kwa sababu ya mila na desturi,” anasema Sarwati.