UTITIRI wa vizuizi vya ukaguzi (beria), imeelezwa ni chanzo kikuu cha rushwa mkoani Kagera, ambapo mtumishi mmoja ndani ya saa tatu anachukua rushwa ya Sh 960,000, ikiwa ni wastani wa Sh 320,000 kwa saa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila katika Mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana ambae yupo mkoani Kagera kukagua miradi ya serikali na uhai wa chama.
Chalamila amesema baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), wanaohudumu vituo hivyo wamekuwa sio waaminifu wanavitumia vibaya kwa kutoza faini za juu kwa wasafirishaji, jambo ambalo humlazimu mtozwa faini kutafuta mbadala wa kukwepa faini, hivyo kujengeka mazingira ya rushwa kirahisi.
“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti (Kinana), Mkoa huu una utitiri wa beria na ni chanzo kikuu cha ‘mchwa’, wanakamata vitu vya watu mpaka mikungu ya ndizi, kesho yake ukienda haipo.
“Maduka mengi ya Watanzania Mtukula yapo upande wa Uganda, huku upande wa Tanzania hamna, leo hii saa tatu na nusu kuna mtumishi amechukua rushwa ya shilingi 960,000 kwa maana nyingine mtu huyo amechukua 320,000 kwa kila saa moja, ndani ya saa tatu kashakusanya kiasi hicho cha fedha.
“Wapo 14, Jumatatu mtapata majibu yao…..wanatengeneza mazingira magumu kwa wafanyabiashara, ili tu wapate rushwa,” amesema.
Amesema tayari ameshaanza kuchukua hatua kwa kuunda kamati ndogo na baadhi ya beria zitapunguzwa.
Kauli ya Chalamila imekuja kufuatia malalamiko mengi yaliyotolewa na wafanyabiashara kwa Kinana, ambaye alitaka kujua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa mkoa huo.
Katika mkutano huo, wafanyabiashara hao walilalamikia utitiri wa beria zilizopo barabarani, unapoingia na kutoka Tanzania kupitia mpaka wa Uganda, eneo la Mtukula.
Eneo lilalolalamikiwa zaidi ni kutokea Mtukula hadi Bukoba mjini ambapo kuna wingi wa vituo njiani.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Jane Charles alisema kutokea Mtukula hadi Bukoba Mjini kuna beria zaidi ya tisa upande wa Tanzania, lakini ukiingia Uganda hadi mjini kuna beria moja…na kibaya zaidi ukiangalia beria hizo nyingine zinafanya kazi sawa na beria zingine na kudai kuwa ni usumbufu kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wa Kinana akizungumzia hilo alisema: “Hata mimi nimeziona beria ni nyingi, nikipita zinafunguliwa, nikivuka zinafungwa, mtu gunia moja anaulizwa kodi, hata kuuza hajauza, sisemi msikate tozo ila ziwe rafiki.”
Amesema atakutana na wabunge wote wa mikoa ya mipakani Kilimanjaro, Katavi, Kagera, Kigoma, Mbeya na kuzungumza nao ili hatua zaidi kuchukuliwa.