Chalamila: Nina bahati kuhamishiwa Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema anajisikia mwenye bahati kuhamishiwa katika mkoa huo.
Chalamila alisema jana jioni kuwa ana deni kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kufikia malengo ya kuufanya mkoa huo kitovu cha biashara.
“Kwanza nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua, hakuna uteuzi mdogo, uteuzi wowote unaofanywa na rais ni mkubwa sana. Mimi namshukuru na jana (juzi) amenihamisha kutoka Kagera kuja Dar es Salaam, amenipa imani kubwa nina deni,” alisema alipozungumza na HabariLEO.
Chalamila alisema anajisikia mwenye bahati kwa kuwa yeyote angeweza kuhamishiwa Dar es Salaam Rais Samia akaamua kumpeleka yeye.
Amemuahidi Rais Samia kuwa atafanya kazi kwa bidii, kujituma na kushirikiana ili kuhakikisha lengo la kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha biashara linatimizwa na kulindwa.
Aliwaeleza wananchi wa mkoa huo kuwa mlango uko wazi na kuwaomba wampe mawazo yenye tija kuendeleza mkoa huo.
Awali, Chalamila alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera na aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mbeya.
Juzi Rais Samia Suluhu Hassan alihamisha wakuu wa mikoa minne akiwamo Chalamila.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Zuhura alieleza katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Chalamila anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Taarifa ilieleza kuwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Zuhura alieleza kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
“Uhamisho huu wa wakuu wa mikoa unaanza mara moja,” alieleza.
Wakati huo huo, Chalamila alifanya ziara ya kustukiza katika Soko la Mwenge ikiwa ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo baada ya kuhamishwa kituo cha kazi na Rais Samia kutoka Kagera.
Akizungumza baada ya kufika katika Soko hilo jana alisema dhamira ya kupita kwenye maduka mbalimbali ni kuona hali halisi ya kinachozungumzwa na wafanyabiashara mitaani.
“Pamoja na kuwa sijaingia ofisini rasmi lakini nimeona ipo haja ya kusikia hasa huku mtaani watu wanasema nini, lakini katika moja eneo nililopita watu wanalalamikia uwepo wa kodi kubwa zisizoweza kulipwa na wafanyabiashara kutokana na kiwango kikubwa cha VAT ambayo ni asilimia 18,” alisema.
Aidha Chalamila alisema suala jingine ambalo linalalamikiwa na wafanyabiashara hao ni kuhusiana na d
idara ya forodha ambayo imeweka viwango vikubwa vya kodi hasa katika vitenge pamoja na mlolongo mrefu wa Ufuatiliaji ambapo ni kikwazo kwa wafanyabiashara wengi.
“Jambo la tatu ambalo nimelisikia ni kuwepo kwa zoezi la kamata kamata kwa wafanyabiashara Kariakoo na kuwakosesha uhuru pamoja na kuleta usumbufu kwa wateja wao na hasa kwa wateja kutoka Kongo, Zambia, Malawi pamoja na mataifa mengine,” alisema.
Pia mkuu huyo wa mkoa alisema kingine alichobaini kwa wafanyabiashara katika eneo la Mwenge ni kuwepo kwa wafanyakazi wanafunzi ambao wanatumiwa na TRA ambao wanakuwa hawana uwezo wa lugha nzuri na yenye staha kwa wafanyabiashara.
“Jambo jingine ni utaratibu wa TRA kuruhusu mizigo kutoka bandarini na baadaye tena wanakuja kukagua nyaraka sehemu za kuhifadhia mizigo (Godown), jambo ambalo wafanyabiashara wanasema ni usumbufu mkubwa kwao”.