Chalinze Cement yaishitaki Brela kufutiwa leseni

KAMPUNI ya Saruji ya Chalinze imefungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu Masijala Kuu Dar es Salaam, dhidi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ikipinga kufutiwa usajili wake.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo na mwanahisa, Mohamed Bahadela akiwa mwombaji wa pili katika kesi hiyo namba 113/2023, pamoja na mambo mengine wameiomba mahakama iamuru kwamba mwombaji wa kwanza (Chalinze Cement) irejeshwe kwenye orodha za kampuni.

Pia waliomba mahakama hiyo itoe amri nyingine yoyote au afueni ambayo itaona inafaa kwa kuzingatia haki na usawa.

Katika hati ya kiapo iliyoandaliwa na waombaji hao chini ya Law Associates Advocates, wanadai kwamba Brela ndio yenye mamlaka ya kusajili na kuziondolea usajili kampuni nchini na ina jukumu la kutunza kumbukumbu zote za kampuni.

Wanadai kuwa kampuni ya Chalinze ilisajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kupewa namba za usajili 154321420 Desemba 3, 2021.

Wanadai kuwa kampuni hiyo ilisajiliwa kwa ajili ya kufanya biashara hususani katika uzalishaji, usafirishaji, uagizaji na uuzaji wa saruji, vifaa vya ujenzi na mashine.

Pia wanadai wana leseni ya uchimbaji kwa eneo ambalo wangefanyia shughuli zao na kwamba wamekuwa wakifuata sheria na kanuni za utunzaji wa mazingira bila kusababisha changamoto au kutokuelewana kati yao na mamlaka za serikali.

Kampuni hiyo inadai kuwa wameshtushwa na taarifa za kufutiwa usajili zilizochapishwa na gazeti la Jamhuri Aprili 25, mwaka huu na kwamba katika taarifa hiyo ilionesha kwamba kampuni ilifutiwa usajili wake tangu Machi 3, mwaka huu.

Walidai baada ya taarifa hizo, walifanya ufuatiliaji na kubaini kwamba Brela imeondoa usajili wao na kuchapisha kwenye gazeti la Serikali Machi 3, mwaka huu.

Waliendelea kudai kuwa hawakuwa na taarifa wala notisi kuhusu kufutiwa kwao usajili licha ya kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Wanadai kuwa kampuni hiyo inaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji kwa maendeleo kabla ya kufutiwa usajili.

Wanadai kuwa wamehuzunishwa na maamuzi ya Brela ya kuwaondolea usajili bila kuwapa notisi wala kuwasikiliza.

“Kwa hali ilivyo, madhumuni ya ombi hili ni kumuagiza Msajili wa kampuni kuirejesha kampuni hii ili aweze kuendelea kufanya biashara zake na shughuli nyingine zozote zinazolenga kukuza biashara na uwekezaji,” walidai.

Kampuni hiyo inahusishwa na kutotaka muunganiko wa kampuni za saruji nchini za Tanga na Twiga kuungana hivyo kukwamisha mchakato huo.

Muunganiko huo ulianza Oktoba 2021, wakati Scancem International DA (Scancem) ambayo ni kampuni tanzu ya Heidelberg Cement AG inayomiliki Twiga Cement na AfriSam Mauritius Investment Holdings Limited, mmiliki wa Tanga Cement zilipotoa taarifa ya pamoja kuwa zimekamilisha masharti ambayo awali Twiga angepata asilimia 68.33 ya hisa kutoka Tanga Cement.

Tume ya Ushindani (FCC) iliidhinisha uamuzi huo, lakini ulibatilishwa na Mahakama ya Ushindani wa Haki (FCT) katika uamuzi wake wa Septemba 23, 2022, baada ya Kampuni ya Chalinze Cement Limited na Jumuiya ya Kutetea Watumiaji Tanzania (TCAS) kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Hata hivyo, akielezea sababu za kufutwa kwa kampuni hiyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Ashatu Kijaji alisema notisi ya kusudio la kufutwa kwa kampuni hiyo ilitolewa Januari 19, 2023, lakini hadi siku hizo zilipomalizika, hakukuwa na maelezo yaliyopokelewa.

“Anuani ya kampuni haipo kwenye usajili popote pale ndani ya Taifa kwa hiyo anuani ni ya uongo na hivyo huwezi kumfikia kwa sababu hujui yuko wapi anuani za wanahisa alizozisajili hazipo, kwa hiyo ni wakufikirika.

“Mawasiliano ya simu yaliyosajiliwa sio ya mwanahisa aliyetajwa kwenye kampuni hiyo,” alisema Dk Kijaji.

Habari Zifananazo

Back to top button