Chama, Yanga ndoto za Abunuwasi

DAR ES SALAAM: KITENDAWILI cha hatma wa kiungo wa Klabu ya Simba, Clatous Chama kimeteguliwa baada ya nyota huyo kuongeza mkataba wa miaka miwili kusalia ndani ya kikosi cha wekundu hao wa Msimbazi kwa msimu ujao wa mashindano.

Chama mkataba wake umefikia ukingoni na ilidaiwa kuwa nyota huyo amekuwa na mazungumzo na Rais wa klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said kwa ajili ya kusajiliwa na Mabingwa wa Ligi Kuu Bara mara 30, Yanga SC.

SOMA: Chama? Yanga wafunguka

Advertisement

Taarifa zinaeleza kuwa, Chama amesaini mkataba wa miaka miwili kusalia unyamani, na uvumi wa kuhusishwa na Yanga umekuwa nit endo la mazoea kwa kila misimu kuhusishwa na pacha wa Kariakoo.

Spotileo leo imemtafuta Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally na kueleza kuwa watawamuongezea mkataba mchezaji yeyote atakayehitajika kusalia katika kikosi hicho.

Amesema haishindwi kumuongezea mkataba mchezaji mwenye malengo naye kwa sababu ya kifedha bali mchezaji atakaye ondoka ni mwenyewe akitaka kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.

“Mchezaji yoyote Simba tunahitaji kubaki naye msimu ujao basi tutatoa gharama yoyote tutambakiza isipokuwa yule ambaye atakuwa amepata ofa nyingine na sio ndani hapa.

Mwekezaji na Rais wa Heshima, Mohamed Dewji ameweka mzigo mezani, hakuna mchezaji anayetakiwa na Simba akaondoka kisa fedha. Huyo Chama wamekuwa wakimsajili kila msimu na anabaki katika viunga vya Msimbazi,” amesema Ofisa habari  huyo.

Ameongeza kuwa usajili wa safari hii upo kwenye mikono salama ukisimamiwa kwa umakini Mo Dewji kuhakikisha wanafanya usajili mzuri kwa kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa kombe la Shirikisho la Afrika (CAFCC).

Ahmed amewataka mashabiki kuwa watulivu, na kukiri kuwa wanafahamu ya kuwa msimu huu hawakufanya vizuri na watarejea ripoti zilizoandaliwa na wataalamu wao ili kusahihisha makosa ya ikiwemo kufanya usajili wa wachezaji bora watakaowapa matokeo.

Simba msimu huu hawakufanya vizuri kwenye ligi, hivyo kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo hali inayowafanya kupoteza nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) msimu ujao badala yake kuibukia CAFCC.

Pia, msimu huu, Simba imeondolewa katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRBD dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma walikuwa wenyeji wa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika.