DAR ES SALAAM – KIUNGO wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua ameisihi klabu hiyo kusajili wachezaji chipukizi wenye ubora kwa ajili ya msimu ujao.
Chambua aliyetamba na Yanga mwanzoni mwa miaka ya 1990 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 2000, alisema klabu hiyo ina wachezaji wengi wenye umri mkubwa hivyo wanapaswa kusajili damu changa wakati huu.
Aliwataja wachezaji Salum Abubakari, Jonas Mkude na Khalid Aucho kuwa umri wao umeenda na kwamba hawana muda mrefu wa kuitumikia timu hiyo.
“Ubora wa Yanga msimu ujao utategemea kama watasajili wachezaji chipukizi wenye uwezo hasa katika eneo la kiungo kuchukua nafasi za kina Sure Boy, Mkude na Aucho,” alisema Chambua.
Alitaja maeneo mengine ya kuimarishwa kuwa ni la beki wa kati na eneo la ushambuliaji.
Alisema bado Yanga inauhitaji wa kusajili beki wa kati mrefu atakayeendana na falsafa ya kocha Miguel Gamondi na kusema nahodha wa timu hiyo Bakari Mwamnyeto amekosa mwendelezo wa kiwango chake.