Changamoto barabara sababu utoro wanafunzi Kingani

UBOVU wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 7, katika shule ya Sekondari Kingani, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, umetajwa kuwa sababu kubwa ya utoro kwa wanafunzi hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu.

Hayo yalibainishwa na makamu mkuu wa shule hiyo, Steven Mbingi, wakati akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula la shule hiyo katika ziara ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo, katika mwendelezo wa mbizo za bendera ya CCM, kata za Kisutu na Nianjema.

Alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 7 kutoka mjini kuelekea katika shule hiyo ni mbovu na kushindwa kupitika katika misimu yote Kwa mwaka mzima jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa utoro kwa wanafunzi wa kutwa.

“Shule hii inawafunzi wa kutwa na Bweni, lakini ubovu wa barabara unatusumbua sana kudhibiti utoro kwani wanafunzi wa kutwa wanashindwa kufika shuleni kwa wakati wanatembea umbali mrefu hivyo wakifika darasani wanakuwa wachovu kupindukia na wengine wanaishia kuwa watoro”alisema

Aidha aliiomba serikali kutatua changamoto na kuitengeneza barabara hiyo hatua ambayo itaisaidia kukomesha tabia ya utoro na kukuza kiwango cha ufaulu tofauti na ilivyo sasa.

Irene Joshua, ambaye ni mwafunzi wa shule hiyo, alisema ubovu wa barabara hiyo umekuwa ni changamoto kubwa kwao kutokana kushindwa kumudu gharama za usafiri na kusababisha wengine kubaki nyumbani na kushindwa kuhudhuria masomo

Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Abdurashidi Zahoro, wakala wa barabara za mijini na Vijijini TARURA, uitengeneza barabara hiyo kwa wakati hatua ambayo itawasaidia wanafunzi kuondokana na adha hiyo na kukomesha utoro.

“Kamati ya siasa tumeagiza barabara hii itengezwe haraka kwani serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi na kuwekeza katika elimu ni muhimu tutambue hilo na mambo madogo kama haya yasije kufifisha lengo la serikali katika uboreshaji wa sekta ya elimu”alisema

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Muharami Mkenge, alisema serikali kupitia TARURA katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 imeshatenga fedha za kukarabati na kutengeza barabara zote muhimu katika jimbo hilo ikiwemo barabara hiyo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button