KATAVI; Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, imetenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha utakaoanza Julai mosi mwaka huu kwa ajili ya kutatua changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo iliyopo Shule ya Sekondari Mnyagala.
Hatua hiyo inatokana na changamoto iliyowasilishwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Mnyagala, iliyopo Kata ya Mnyagala ambao wameomba serikali kuwaongezea miundombinu ya vyoo, kwani matundu yaliyopo hayatoshelezi mahitaji hali inayowafanya kukosa umakini wa masomo wawapo darasani.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko baada ya kutembelea shuleni hapo, mwanafunzi wa kidato cha nne Victoria Noja, amesema licha ya serikali kukamilisha ujenzi wa shule
hiyo lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya matundu ya vyoo.
“Matundu ya vyoo yaliyopo ni 6, lakini wanafunzi tuliopo ni wengi sana,” amesema Victoria na kuiomba serikali kuwajengea matundu zaidi.
Akijibu hoja hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika, Dk Alex Mrema amesema wanatambua changamoto ya matundu ya vyoo katika shule hiyo na kwamba kabla ya kufikia muda huo watajadiliana na ofisa Mipango endapo wanaweza kujenga vyoo hivyo, ili ujenzi huo kuanza kabla ya mwezi Julai ili kutatua changamoto hiyo haraka iwezekanavyo.