Changamoto somo la hisabati kupatiwa ufumbuzi
SERIKALI imeanza kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ufaulu mdogo kwenye somo la hisabati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.
Hatua hiyo ni kuanza kwa mpango wa kutolewa mafunzo maalumu ya ufundishaji kwa njia ya Tehema kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu ambayo yatasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu wa somo hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ,Profesa Carolyne Nombo, alisema hayo Julai 11, 2023 mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo kwa wakufuzi wa vyuo vya ualimu nchini wa somo la hisabati, ukiwa utekelezaji wa kuimarisha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo.
Mafunzo hayo ya siku tano yameshirikisha wakufunzi 155 wa vyuo vya ualimu kutoka Kanda ya Kaskazini, Mashariki, Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi ,Kanda ya Kati na Kanda ya Kusini.
Profesa Nombo alisema hatua hiyo ya kutumia Tehema hasa ni katika kipindi hiki ambako serikali inatekeleza mageuzi makubwa ya uboreshaji wa elimu nchini.
Katibu mkuu huyo alisema katika kufanikisha mpango wa kuinua ufaulu wa somo la hisabati, serikali kupitia wizara hiyo tayari imewekeza za katika ujenzi wa majengo mapya na kuimarisha miundombinu ikiwemo maabara na kuanzisha majengo mapya ya tehema kila chuo cha ualimu.
“Kumekuwa na changamoto ya ufaulu wa somo la hisabati na mazingira ya kufundishia sio mazuri na serikali yetu imeamua kuweza kwa kiwango kikubwa kwenye vyuo vya ualimu ili viweze kutoa walimu watakaofundisha somo hilo katika shule za msingi na sekondari.” alisema Profesa Nombo.
Profesa Nombo alisema tayari serikali imewekeza kwa kujenga kituo cha sayansi katika Chuo cha Ualimu Morogoro chenye vifaa mbalimbali vya kisasa vya kitehema.
Alitaja vifaa hivyo ni pamoja na vishkwambi, kompyuta ambazo vinazowezesha wakufunzi wa vyuo vya uwalimu kujifunza hata wakiwa nje ya vituo vyao.
Profesa Nombo alisema, wakufunzi hao watapitishwa kwenye matumizi ya mifumo mizuri ya somo la hisabati ,matumizi mazuri ya vishikwambi kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia wao wenyewe na kujengewa mbinu za kufundisha hisabati kwa kutumia Tehema.
Hivyo alisema ni matarajio ya wizara baada ya mafunzo hayo watakwenda kuwawezesha walimu tarajali ambao kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuinua viwango vya ufaulu wa somo hilo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Ualimu , Huruma Mageni, alisema wizara inaendelea na utekelezaji wa kazi mbalimbali za mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) na miongoni mwao ni utoaji wa mafunzo kazini kwa wakufunzi wanaofundisha somo la hisabati.