DAR ES SALAAM: BONDIA Yusuf Changarawe ametamba kupambana katika mashindano ya kufuzu yanayofanyika nchini Italia ili kupata nafasi ya kushiriki michezo ya 33 ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa mwaka huu.
Mashindano hayo ya ndondi ya dunia kufuzu Olimpiki yatafanyika Busto Arsizio nchini Italia kuanzia Machi Mosi-12, 2024 na kuna jumla ya nafasi 49, zikiwemo 28 za wanaume na 21 kwa wanawake.
Changarawe ambaye alishiriki mashindano ya kufuzu ya Afrika kwa Olimpiki 2024 yaliyofanyika Dakar, Senegal mwaka jana, atashindana katika uzani wa kati na katika uzito huo wanawania nafasi nne za kufuzu.