Chanjo ya polio yashika kasi

UTOAJI wa chanjo ya matone ya ugonjwa wa polio umeanza Alhamis nchi nzima huku ukionekana kushika kasi kwa wananchi kutoa ushirikiano wa kupeleka watoto wao walio chini ya miaka mitano.

HabariLEO imetembelea maeneo mbalimbali nchini na kushuhudia uzinduzi wa chanjo hiyo huku viongozi kadhaa wakitoa hamasa kwa wananchi juu ya umuhimu wa chanjo hiyo.

Kutoka Arusha, Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji, Dk Baraka Munde alisema watoto 93,218 wanatarajiwa kuchanjwa na kupewa dozi hiyo ya polio.

Advertisement

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda akiwa katika kituo cha afya cha Levolosi alisema polio husababisha ulemavu wa viungo au kushindwa kutembea hivyo ni lazima wazazi na walezi wawapeleke watoto wao kupata chanjo ya polio.

Aliwataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana na serikali katika utoaji chanjo hiyo ya polio na kuongeza. Alisema kampeni hiyo ya uchanjaji itavuka lengo ili kila mtoto apate haki yake muhimu ya kiafya.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko alisema malengo yao ni kuwafikia watoto 88,376 kwa Halmashauri na Manispaa ya Shinyanga ni 44,013.

“Ugonjwa huu ni mbaya, hivyo tusifanye masihara kwani watoto wetu wakipata chanjo ya matone watakuwa salama, wataepuka magonjwa kwa sababu watakuwa na kinga ya kutosha, hawatayumbishwa na ugonjwa huo hata kama walipata chanjo awamu ya kwanza na ya pili haina madhara yoyote wachanjwe,” alisema Mboneko.

Kwa upande wa Mkoa wa Pwani, unatarajia kuchanja watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano zaidi ya 263,990 ili kuwakinga na ugonjwa huo kwa kuwapa matone.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema chanjo hiyo si mara ya kwanza kutolewa nchini hivyo wazazi wahakikishe watoto waliolengwa wanafikiwa.

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Gunini Kamba aliwataka viongozi na watendaji wote wa serikali, vyama vya siasa, dini, taasisi na wadau wote kushirikiana kikamilifu na kuhakikisha watoto wanapata taarifa sahihi juu ya chanjo na umuhimu wake.

Alisema katika kuhakikisha kila mtoto anafikiwa, timu za uchanjaji zitapita nyumba kwa nyumba na sehemu yoyote walipo watoto ikiwamo nyumba za ibada chini ya kaulimbiu ‘Kila tone la chanjo ya polio litaiweka Tanzania salama dhidi ya ugonjwa wa kupooza’.

Ofisa Mipango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Immaculate Dotto alisema lengo la kampeni ya chanjo ya polio awamu ya tatu ni kukinga watoto walio chini ya miaka mitano dhidi ya virusi vya ugonjwa huo unaoambukizwa kwa njia ya vinyesi vinavyozagaa ovyo.